Na Baraka Mpenja
Baada ya Prisons na Yanga kuunguruma katika michezo
yao ya jana, leo kipute kingine cha kukata na shoka ni uwanja wa taifa
ambapo wekundu wa msimbazi Simba `Taifa Kubwa` wakiwa ya kocha Mfaransa
Patrick Liewig watakuwa kibaruani kupepetana na Azam fc maarufu kama
wana Lambalamba wanaonolewa na kocha Mwiingereza Sterwart Jan Hall.
Mtanange huo umevuta hisia za mashabiki wa soka kutokana na kuibuka upinzani mkubwa baina ya timu hizo mbili.
Mechi ya mzunguko wa kwanza mwaka jana, Azam
walipoteza mchezo baada ya kukubali kipondo cha mabao 3-2 wakati kipindi
cha kwanza walikuwa wanaongoza 2-0, lakini kimbembe kiliwaangukia
kipindi cha pili baada ya Mnyama kusawazisha yote na kutia kambani
msumari wa ushindi.
Baada ya mechi ile baadhi ya wachezaji wa Azam walikalia kuti la moto kwa tuhumu za kula rushwa kutoka kwa Simba.
Wachezaji hao ni mabeki Aggrey Morris, Said Morad,
na Erasto Nyoni, pia mlinda mlango namba moja kwa wakati ule Deogratius
Munish `Dida` alikumbwa na tuhuma hizo.
Azam waliwapeleka wachezaji hao TAKUKURU lakini
hivi karibuni taasisi hiyo ilitangaza kuwa uchunguzi umeshindwa kubaini
kama kweli walikula mlungula hivyo iliwaachia huru.
Sasa Azam wamewajumuisha nyota hao katika kikosi
chao na kinachosubiriwa ni maamuzi ya kocha kuwapanga katika kipute cha
leo ama la.
Kuelekea katika mchezo huo kila timu imesema
maandalizi yamekamilika na kinachosubiriwa ni muda kufika ili shughuli
ianze uwanjani.
Azam fc kupitia kwa Afisa habari wake Jafar Idd
Maganga walisema maandalizi ya mtanange huo yamekamili, wachezaji wote
wapo salama na wana morali kubwa ya kupata pointi tatu muhimu ili
kuwasogelea Yanga waliopo kileleni kwa pointi 52 sasa baada ya jana
kushinda dhidi ya Oljoro.
“Sisi kila mechi kwetu ni fainali, tunajiandaa
kukabiliana na Simba ambao wameshapoteza ubingwa wao na sasa wanaiwinda
nafasi ya pili, tunalifahamu hilo na ndio maana tumejipanga barabara
kukabiliana nao leo”. Alisema Idd.
Idd aliongeza kuwa Simba wana timu nzuri ambayo inaweza kupata matokeo ya ushindi ingawa kuna baadhi ya watu wanawabeza.
“Wapinzani wetu wanawatumia vyema vijana wao, licha
ya kutokuwa na matokeo mazuri mechi mbili zilizopita bado wanaweza
kufanya lolote, lakini tuko kikosi kamili kwani wachezaji wote wapo
salama kuumana na Mnyama”. Alijinasibu Idd.
Wakati Azam wakijigamba kutumia vyema mchezo huo,
kwa upande wa Simba wamesema wamejiandaa vizuri kupambana na wapinzani
wao ambao wana moto wa kushiriki michuano ya kimataifa.
Akizungumza na matandao huu kocha msaidizi wa Simba
Jamhuri Kiwhelu Julio, alisema kwanza wanamshukuru mungu mwingi wa
rehema kwani kikosi kipo salama kukabiliana wapinzani wao.
Julio alisisitiza kauli yake kwamba Mashabiki wa
Simba wawe na subiri baada ya kupoteza taji lao msimu huu kwani Simba
hii wanayoidharau wataipenda tu msimu ujao.
“Vijana tunaowatumia wanafanya vizuri sana na kama
wataenedelea kujiamini watawabeba sana wana msimbazi. Azam ni wazuri
lakini hatukati tamaa hata kidogo tutapambana nao kufa na kupona ili
angalau tushike nafasi ya pili”. Alisema Julio.
Kocha huyo aliyejaaliwa kuwa na maneno mengi
aliongeza kuwa mashabiki wa simba wajitokeze kwa wingi leo hii
kuwashuhudiwa vijana wao wakifanya kazi nzuri ndani ya dimba murua la
taifa maeneo ya Chang`ombe jijini Dar es salaam.
0 comments:
Post a Comment