Na Supersport.com
Mabingwa watetezi wa kombe la FA nchini
England watakuwa kibaruani leo hii majira ya saa 12 jioni katika uwanja
wa taifa wa Wembley kupepetana na mabingwa watetezi wa taji la ligi kuu
soka nchini England, klabu ya Manchester city mchezo wa nusu fainali ya
pili ya FA.
Miamba hiyo imeshindwa kupambana na
mashetani wekundu kuwania taji la ligi kuu msimu huu ingawa Chelsea
wamefika hatua ya nusu fainali ya ligi ya UROPA, lakini mchezo huu
utakuwa muhimu kwao wote ili kumaliza msimu angalau na kikombe kimoja.
Mshindi wa mchezo wa leo utakumbana
naWigan Athletic katika mtanange wa fainali baada ya klabu hiyo kuibuka
na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu ya daraja la Championship,
Millwall na kutinga hatua ya fainali.
Kocha wa muda wa Chelsea Rafael Benitez na
wa City Roberto Mancini wote kwa pamoja wanawania kutwaa kombe kwa
mara ya pili wakifanya kazi nchini Uingereza.
Mwishoni mwa mwezi februari mwaka huu timu
hizo zilikutana katika dimba la Etihad katika mchezo wa ligi kuu na
kushuhudia City wakiwabamiza wapinzani wao mabao 2-0, lakini Benetez
amesema amejifunza kwa kiasi kikubwa.
“Tunajua itakuwa mechi ngumu, lakini ni
nusu fainali yenye ushindani mkubwa”. Alisema Mhispania huyo aliyetwaa
ubingwa wa kombe hilo mwaka 2006 akiwa na wekundu wa Anfield, klabu ya
Liverpool.
Benetez aliongeza kuwa City ni timu nzuri,
ina kikosi bora na kocha mzuri mwenye uzoefu mkubwa, lakini watajituma
zaidi endapo wanataka kuibuka kidedea katika kipute hicho.
City wanaingia uwanjani wakiwa na
kumbukumbu nzuri ya kuwafumua watani zao wa jadi Manchester United mabao
2-1 katika uwanja wa Old Traford jumatatu ya wiki hii mchezo wa ligi
kuu soka Uingereza.
Mancini amekuwa na presha kubwa baada ya
kuweka rehani ubingwa wake mbele ya united, lakini bado ana nafasi ya
kujikusanyia kombe la tatu ndani ya miaka mitatu.
Kocha huyo aliondoa ukame wa City kutotwaa
ubingwa wa kombe la FA kwa miaka 35 baada ya kuiongoza klabu yake
kunyakua ubingwa mwaka 2011 akiwafunga Stoke city mchezo wa fainali.
Mancini alisema, “nadhani kucheza Wembley
ni bonge la mechi kwa mashabiki wote wa soka hivyo ni nafasi muhimu
kushuhudia mechi hiyo ya nusu fainali”.
Kocha huyo aliongeza kuwa kila kombe ni
muhimu kwa timu zote, lakini kwa upande wao ni muhimu zaidi kwani wana
nafasi ya kutinga fainali na kubeba kombe hilo kwa mara ya pili ndani ya
miaka mitatu.
0 comments:
Post a Comment