Na Baraka Mpenja
Sekunde, dakika, saa zazidi kukatika
kuelekea mpambano mkali wa ligi kuu soka Tanzania bara baina ya mabingwa
watetezi wa ligi hiyo wekundu wa msimbazi Simba dhidi ya mabingwa mara
mbili wa kombe la mapinduzi na wawakilishi pekee wa Tanzania katika
michuano ya kimataifa, Azam fc kwenye uwanja wa kisasa wa taifa jijini
Dar es salaam.
Azam fc na Simba kwasasa zina upinzani mkubwa sana na kila zinapokutana hakika kipute kinakuwa kikali zaidi ya kawaida.
Simba wanaingiwa uwanjani wakiwa tayari
wameshapoteza ubingwa na sasa wanahitaji hata nafasi ya pili ili kupata
nafasi ya kucheza mashindano ya kimataifa mwakani wakati lambalamba wao
wapo nafasi ya pili na pointi 46 wakihitaji kushinda ili kwasogelea
vinara wa ligi hiyo Dar Young Africans.
Kikosi cha Azam kinaonekana kuwa imara
zaidi msimu huu kutokana na matokeo wanayopata katika mechi za ligi kuu
na michuano ya kombe la shirikisho, wakati Mnyama pori anahaha kweli
kutengeneza kikosi kipya baada ya wachezaji wengi `Mafaza` kutemwa na
kocha wake Patrick Liewig kwa makosa ya utovu wa nidhamu.
Mechi tatu zilizopita Simba ilicheza
bila wakongwe wake, Mwinyi Kazimoto Mwitula, Amir Maftah, Ramadhan
Chombo `Redondo`, Haruna Moshi Shaban `Boban`, Ferlix Mumba Sunzu,
Komanbil Keita, Juma Said Nyoso na Abdallah Juma baada ya kocha Liewig
kuwapiga chini.
Wachezaji Juma Kaseja, Mrisho Khalfan
Ngasa `Anko`, Amri Athman Kiemba, Shomary Kapombe Jr, Masoud Nassor
Cholo, walibakishwa kwenye kikosi hicho na kucheza michezo yote mitatu
dhidi ya Coastal union, Kagera Sugar na Toto Africa.
Kwa sasa Kazimoto na Sunzu wamerejeshwa
katika kikosi cha Simba na wanaweza kucheza katika mchezo wa leo endapo
mwalimu utapiga hesabu zake vizuri.
Kwa upande wa Azam fc , wao wako kamili
kado baada ya nyota wake Said Morad, Erasto Nyoni, Aggrey Morris,
Deogratius Munish `Dida` kurejeshwa kikosini baada ya TAKUKURU kushindwa
kuwakuta na hatia ya kula mlungula kama walivyoshitakiwa na klabu yao.
Mbali na nyota hao kuwepo, klabu hiyo
ina wachezaji hatari katika kufumania nyavu, John Rafael Bocco, Brian
Umony, Hamphrey Mieno na Kipre Herman Tchetche.
Lakini wapo wengine machachari kama
Abubakar Salum `Sure Boy`, Michael Bolou, Himid Mao, David Mwantika,
Khamis Mcha `Vialli` na wengineo.
Hakika mpambano huu ni mkali sana na
timu zote zitahitaji ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya msimamo
wa ligi kuu soka Tanzaniania bara inayoelekea ukingoni.
0 comments:
Post a Comment