“Sijawahi kukata tamaa kwenye maisha yangu, kila siku napambana
kufika sehemu ambayo naamini nastahili niwe na ninaamini ipo siku
nitafika huko,” anasema Abasarim Chidiebere ambaye amesaini mkataba wa
miaka miwili na klabu ya Caps United ya Zimbabwe.
“Tangu nilipokuja Tanzania, sijawahi kurudi nyumbani kwetu Nigeria,
yote ni kwa sababu bado naamini natakiwa kupambana zaidi ili kufikia
malengo yangu.”
Chidiebere amesema, sio kama hapendi kwenda kwao lakini haendi
nyumbani kwa sababu bado malengo yake hayajatimia ya kucheza soka la
kulipwa kwenye timu ya ndoto yake ambayo itampa mafanikio ya kutwaa
mataji na kujulikana Afrika nzima pamoja na duniani.
“Akilini kwangu ninajua kwamba siku moja nitaenda nyumbani Nigeria na
kukutana na familia yangu, nimekuwa nikiwasiliana nao mara kwa mara
kuwajulia hali na kuwaambia maendeleo yangu nikiwa huku nchi za
ugenini.”
Nimemuuliza Chid ilikuwaje akapata timu Zimbabwe wakati akiwa hapa
nyumbani hakuna klabu iliyoonesha kumuhitaji kwa ajili ya msimu ujao
mara baada ya mkataba wake na Stand kumalizika.
“Nina agent wangu ambaye ndio anashughulikia mambo yangu mengi ya nje
ya uwanja, alinitafutia timu nikaalikwa Zimbabwe na klabu ya Caps
United kwa ajili ya kufanya majaribio. Nilipofika hapa nilifanya kila
ninachoweza ili nipate nafasi ya kupewa mkataba na hatimaye imekuwa
hivyo.”
“Mimi niliamua kuanzia Tanzania kucheza soka langu kimataifa na
ninashukuru kupitia Tanzania nimeweza kuvuka na kusogea mbele kidogo,
Tanzania bado ni nyumbani kwangu kwa sababu nimepata mke hapa na mtoto
pia.”
“Chidiebere amesema kwa sasa yupo pekeake Zimbabwe anaendea
kukamilisha baadhi ya taratibu na kila kitu kikiwa sawa atakuja
kuichukua familia yake (mke wake Tabitha na mtoto wao Chinonso).”
0 comments:
Post a Comment