YANGA imezidi kushushiwa neema baada ya kuelekezwa kufanya kila inaloweza kumsajili mshambuliaji hatari raia wa Zimbabwe, Rodrick Mutuma, ili kuifanya safu yao ya ushambuliaji kuwa hatari zaidi msimu ujao inapotarajiwa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mutuma ndiye mshambuliaji tegemeo katika kikosi cha timu ya Taifa ya Zimbabwe mwenye uwezo wa hali ya juu wa kucheka na nyavu, zaidi ya ilivyo kwa wakali wa Yanga, Donald Ngoma na Amissi Tambwe.
Mkali huyo mwenye nguvu za kupambana na akili ya mpira, ni miongoni mwa walioonyesha uwezo wa hali ya juu katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) mapema mwaka huu nchini Rwanda.
Kiungo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay, ndiye aliyetoa ushauri kwa timu yake hiyo aliyoichezea kwa mafanikio makubwa, akiamini Mutuma anaweza kuwa ‘pacha’ mzuri wa Ngoma.
Mayay alisema amekiangalia kwa umakini kikosi cha Yanga akiamini kimekamilika kila idara, isipokuwa bado inahitaji mshambuliaji mmoja aina ya Ngoma ili kuweza kujiweka katika mazingira mazuri ya kufika mbali katika michuano ya kimataifa.
“Yanga wana timu nzuri, lakini ukweli kwamba sasa hivi wakimkosa Ngoma, wanakuwa katika wakati mgumu, nafikiri benchi la ufundi linahitaji utulivu kidogo kutafuta mtu sahihi ambaye anaweza kuziba vyema pengo la Ngoma endapo anakosekana katika kikosi,” alisema Mayay.
Alisema kwa kipindi hiki hakuna wachezaji wazawa wenye uwezo wa kuichezea Yanga kutokana na ukweli kwamba mabingwa hao wanahitaji wachezaji walio katika viwango vya juu kuweza kutimiza ndoto zao za kufika mbali kimataifa.
“Kwa hapa nyumbani hakuna mshambuliaji kutoka katika timu yoyote inayoshiriki katika Ligi Kuu anaweza kuziba pengo la Ngoma bado sijaona, labda nje ya nchi kama Malawi, Zambia na Zimbabwe, kule kuna wachezaji wazuri sana zaidi ya 1,000,” alisisitiza Mayay.
Mayay alisema kwa upande wake, Mutuma anamuona anaweza kuwa mbadala wa Ngoma endapo itatokea amepata majeraha au adhabu ya kutumikia kutokana na uwezo mkubwa alionao.
“Yule jamaa ni mshambuliaji hasa, Ngoma mwenyewe anamjua, muulizeni atawaambia; ana uwezo wa kupambana na kila aina ya beki, ana nguvu, ni mjanja, anajua kupambana mwanzo mwisho. Ana kila aina ya sifa kama ya Ngoma,” alisema Mayay.
Nahodha huyo wa zamani wa Yanga alisema amekuwa akimfuatilia kwa karibu mshambuliaji huyo na kugundua ana vitu vingi adimu ambavyo wachezaji wengi wa Tanzania wa sasa wanakosa kutokana na kushindwa kwao kujituma uwanjani.
“Binafsi nimekuwa nikimfuatilia kwa karibu sana na si yeye tu, kuna wengine wengi ambao wanatoka nchi za Zambia, Malawi, Kongo na nyinginezo walicheza katika michuano ya Chan kule Rwanda, lakini huyu Mutuma ni jembe kwa kweli,” alisisitiza Mayay.
Juu ya ushauri huo wa Mayay, tayari klabu ya Yanga imeweka wazi kusaka wachezaji wa kiwango cha juu ili waweze kutimiza ndoto yao ya kutikisa Afrika kwa kufanya kweli kwenye michuano ndani ya bara hilo.
Kwa sasa Yanga inakabiliwa na mchezo wa marudiano wa hatua ya 16 wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Sagrada Esparanca ya Angola utakaopigwa ugenini.
Katika mchezo wa kwanza, Wana-Jangwani hao walishinda mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam hivyo iwapo watashinda au kupata sare ugenini Jumatano, watakuwa wametinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.
0 comments:
Post a Comment