
USHINDI wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji APR kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika, ulifanya msafara wa Yanga kuamua kuwaachia wachezaji wake wajirushe usiku kucha katika klabu ya usiku jijini Kigali.
Yanga ilipata ushindi huo juzi kwenye Uwanja wa Amahoro na kisha baadaye usiku wachezaji wote wakaruhusiwa kujirusha kwenye klabu ya Class iliyopo karibu na hoteli ya kimataifa ya The Mirror ambayo timu hiyo imefikia ambako wachezaji hao walipata vinywaji na kucheza muziki hali ambayo haijawahi kutokea kwa kipindi kirefu katika klabu hiyo.
Wakiwa ndani ya klabu hiyo wachezaji hao walionekana kufurahia ushindi huo kwa namna yake huku wengine wakiwa na hamu ya kufika mbali zaidi msimu huu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakipania kuweka rekodi wakiwa na kikosi cha mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kitendo cha wachezaji wa Yanga kuwemo ndani ya klabu hiyo kulibadili kabisa sura usiku huo kwani shughuli hazikwenda kama ilivyokawaida na zaidi watu walikuwa na shamrashamra na wengine wakiwashangaa wachezaji hao.
Pamoja na hayo, mashabiki wengine wa Yanga waliopo jijini Kigali nao walipata nafasi ya kujumuika na wachezaji hao katika mtoko huo, huku makumi ya mashabiki wengine wakishindwa kuingia katika klabu hiyo kuungana na wachezaji wa Yanga kutokana na ulinzi mkali uliokuwepo.
Chanzo:Bingwa

0 comments:
Post a Comment