
Mrisho Ngasa
KOCHA aliyemsajili Mrisho Ngassa Afrika Kusini,Kinnah Phiri ameweka wazi kwamba mchezaji huyo mambo yake si mazuri na alishatamani hata kurudi kwenye klabu yake ya zamani ya Yanga kwa mkopo.
Ngassa ameondolewa kwenye kikosi cha Taifa Stars kinachojiandaa na mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Chad lakini imebainika kwamba maisha ya soka ya mshambuliaji huyo katika klabu ya Free States ya Afrika Kusini ni magumu.
Kocha wa Stars, Boniface Mkwasa alitangaza kikosi hicho juzi Jumanne huku winga huyo akiwekwa kando kwa kilichoelezwa kuwa ametoka kufanyiwa upasuaji hivi karibuni hivyo hayupo fiti kuwavaa Chad.
Hata hivyo aliyekuwa kocha wa Free States, Kinnah Phiri, raia wa Malawi alisema kuwa maisha ya kisoka kwa Ngassa yamekuwa magumu tangu aondoke kwani amebadilishwa namba aliyokuwa akicheza, sasa anachezeshwa kama kiungo mkabaji na mshambuliaji.
“Huwa nawasiliana na Ngassa, ni mchezaji mzuri ila sasa wanampoteza kwa kumbadilisha nafasi anayocheza, Ngassa ni winga ila kocha aliyepo anamchezesha kiungo mkabaji na kiungo mshambuliaji jambo ambalo ni gumu kwa kwake na anatamani kuondoka huko.
“Nilijaribu kumshauri azungumze na wakala wake ili wawaombe viongozi wa Free States kwasababu mkataba wake ni mrefu, wamtoe kwa mkopo hata timu za hapa Tanzania maana maisha yake yanazidi kuwa magumu na watapoteza kipaji chake, ila ushauri wangu ulionekana kuwa mgumu kwani wakala wake alikataa,” alisema Phiri
Phiri ambaye kwasasa anainoa Mbeya City, alisema kwa mchezaji wa Tanzania kwenda kucheza soka Afrika Kusini humchukua muda mrefu kwenda sawa na mfumo wa kule kwani soka la nchini humo ni profeshono zaidi kuliko hapa nchini.
“Kuna wengine wanaokwenda Afrika Kusini si kutoka Tanzania pekee hata nchini nyingine Afrika Mashariki, wanachukua muda mrefu kwenda sawa na mfumo wa soka la kule, mpira wa Afrika Mashariki kwa asilimia kubwa unafanana tofauti na kule ambako mpira wao unafanana na nchi za Ulaya, hivyo kwa Ngassa lazima atapata tabu maana kuna wakati anacheza na muda mwingine hapewi nafasi kabisa,” alisema Phiri.
Chanzo:Mwanaspoti
0 comments:
Post a Comment