Kwa mara ya kwanza aliyekuwa daktari wa Yanga, Nassor Matuzya amefunguka chanzo cha kutimka kikosini hapo ikiwa ni siku kadhaa baada ya kuchukua jukumu hilo, ambapo ameeleza hali ya mambo ilivyo kwenye utawala wa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, ajira yake imembana.
Matuzya ambaye alichukua nafasi ya Haroun Ally ambaye pia hakukaa sana klabuni hapo, huku kwa sasa ikiwa chini ya Edward Bavu.
Matuzya amelifafanulia Championi Jumatano kuwa ajira yake ipo serikalini katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke na kwa sasa majukumu yameongezeka zaidi yanayomfanya kuwa bize muda mwingi, tofauti na awali.
Alisema awali ilikuwa rahisi kumuachia mfanyakazi mwenzako kukushikia zamu na kuendelea na ishu nyingine zaidi ya ajira rasmi, lakini kipindi hiki cha JPM mambo ni tofauti, ingawa amesisitiza bado yupo tayari kutoa huduma kwa Yanga iwapo atakuwa na muda.
“Nimebanwa na ajira kwa sasa kwa upande wa serikali, kimsingi unajua wakati huu wa Magufuli ni tofauti na wakati mwingine wowote. Kwa sasa kila mtu anataka kujikita kwenye sehemu yake.
“Wakati ule ulikuwa unaweza kumwambia mtu akushikie zamu, lakini kama utakuwa unatoka kila siku ni nani atakuwa tayari kuumia kwa ajili yako? Vinginevyo labda uchukue likizo isiyo na malipo ili ukawasaidie Yanga. Pia mbali na hilo, kwa sasa nafasi yangu imebadilika, majukumu yameongezeka, tofauti na nilivyokuwa Mwananyamala,” alisema Matuzya.
SOURCE: CHAMPIONI
0 comments:
Post a Comment