KIPIGO cha mabao 4-1 walichokipata timu ya Toto African ya Mwanza kutoka kwa Yanga kimemfanya kocha mzungu wa timu hiyo, Martin Grelics kujiuzulu wadhifa wake.
Toto waliokutana na Yanga wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa waliondoka mikono mitupu kwa kukubali kichapo cha bao 4-1 kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Katika barua yake aliyoandika kwa uongozi wa klabu hiyo, kocha Grelics licha ya kutotaja moja kwa moja uhusiano wa kujiuzulu kwake na matokeo ya mechi za hivi karibuni za timu hiyo, lakini alisema anaachia ngazi kutokana na sababu mbalimbali.
“Si kwamba najiuzulu kutokana na matokeo ya mechi za hivi karibuni, lakini kutokana na jinsi mambo yanavyoendeshwa ndani ya klabu, klabu ya soka la kulipwa haiwezi kuendeshwa hivi na mimi kama kocha mwanataaluma nikakubali.
“Naachia ngazi nikiamini kwamba kuondoka kwangu kunaweza kutoa nafasi pengine kwa uongozi kujipanga na kutekeleza mambo muhimu kwa klabu hii ili iweze kusonga mbele,” alisema kocha huyo katika barua yake.
Kocha huyo alitaja sababu kulazimika kuachia ngazi wadhifa huo ni kubeba majukumu ambayo sio yake kiutawala na kutolea mfano suala la mishahara ya wachezaji ambayo haijalipwa miezi mitatu mpaka sasa na kitendo cha kusafiri kwa shida katika safari za timu akitolea mfano wa safari za Tanga na Tabora, ambazo zilikuwa ngumu sana bila kufafanua kwa undani.
0 comments:
Post a Comment