Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania - TFF, Jamal Malinzi leo ameagana rasmi na aliyekua kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, mholanzi Mart Nooij.
Akiongea na waandishi wa habari leo katika hoteli ya Tansoma, Malinzi amesema wameamua kuagana nae mbele ya vyombo ya habari kama iliyofanyika pia wakati wa utambulisho wake wakati wa kuanza kazi.
“Mpira wa miguu unachangamoto nyingi, watanzania tunasafari ndefu katika mafanikio ndio maana TFF imeanza kuwekeza katika soka la vijana, sababu ndio msingi wa kuwa na timu bora ya Taifa” alisema Malinzi.
Duniani kote chimbuko la timu bora ni soka la vijana na watoto, tukiwa na vijana wengi walioanza kucheza mpira katika umri mdogo wanapofikia umri wa kuchezea timu ya Taifa tutakua na kikosi bora.
Nchi za wenzetu inapofikia kocha kuita wachezaji wa timu ya Taifa anakuwa na wigo mpana, kwetu sisi wachezaji wanocheza soka nje ya nchi wanahesabika, hivyo ni lazima tuanze kuwekeza kwenye soka la vijana
TFF ilishaanza mkakati huo ndio maana kuna timu za U13, U15 ambazo zitakua zikiingia kambini na kucheza michezo ya kirafiki ndani ya nje kwa lengo la kupata uzoefu kabla ya kushiriki kuwania kufuzu kwa fainali za vijana mwaka 2016.
Kikosi cha U15 kinatarajiwa kufanya ziara mwezi Disemba mwaka huu katika nchi za Malawi, Zambia, Zimbambwe, Botswana na Afrika Kusini, kisha mwakani mwezi April 2016 kitaenda Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya kucheza michezo ya kirafiki.
Naye Mart Nooij aliyekua kocha wa Taifa Stars, akiongea na waaandishi wa habari alisema anawashukuru watanzania wote, serikali, wadau wa mpira wa miguu nchini na TFF kwa sapoti waliyompatia wakati akiwa kocha mkuu wa timu ya Taifa.
Nooij alisema alifurahia maisha yake akiwa Tanzania kwa kipindi chote alichokua akifundisha timu ya Taifa, lakini kwa sababu imefikia mwisho wa ajira yake hana jinsi anaondoka, lakini ataendelea kuikumbuka Tanzania na watanzania wote kila siku kwa ukarimu wao.
0 comments:
Post a Comment