Nkamia akihutubia jana
Naibu waziri wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Juma Nkamia ameishauri Azam TV kuongeza asilimia 40 ya mapato
yaliyopungua ili vilabu viweze kunufaika tofauti na sasa ambapo timu zinalia
kushuka kwa mapato ya uwanjani.
Nkamia ametoa kauli hiyo jana wakati wa utoaji wa tuzo za
ligi kuu soka Tanzania bara 2014/2015 zilizoandaliwa na Bodi ya ligi kwa
kushirikiana na wadhamini wa ligi, Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom.
“Suala la mapato kushuka limezungumzwa sana, nitoe rai kwa
Azam TV wanaorusha matangazo haya moja kwa moja ya ligi kuongeza ile asilimia
40 ya mapato yaliyopungua ili vilabu viweze kunufaika tofauti na hali
ilivyosasa. Naamini Azam TV ni watu wazuri, wakiongeza hali hiyo mapato
yanaweza kuboreka”. Amesema Nkamia.
Hata hivyo, Nkamia, mtangazaji wa zamani wa mpira wa miguu wa TBC,
amebainisha kwamba upangaji mbovu wa ratiba ya ligi kuu nao huchangia kushuka
kwa mapato ya milangoni.
“Kwa mtazamo wangu, hata upangaji wa ratiba za ligi nao
unachangia kushuka kwa mapato, si rahisi timu kubwa kama Yanga ikacheza mechi
uwanja wa Taifa Jumamosi, halafu Jumapili wacheze Simba ukategemea mapato kukua”.
Aidha, Nkamia amesema wizara inapambana kutafuta suluhu ya
gharama kubwa ya bei za vifaa vya michezo.
“ Kwa upande wetu tunajaribu kuzungumza na Wizara ya Fedha
ili kuangalia namna tunavyoweza kutatua jambo hili, imani yangu ni jambo hili
litatafutiwa ufumbuzi wake”. Nkamia Amethibitisha.
0 comments:
Post a Comment