Uongozi wa chama cha soka visiwani Zanzibar (ZFA) umeridhia uteuzi wa kocha Hemed Morocco kuwa kocha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ atakaefanya kazi chini ya Charles Boniface Mkwasa kufuatia kamati ya utendaji ya TFF kumfukuza kocha pamoja na kulivunja benchi la ufundi lililokuwa likiongozwa na kocha Mart Nooij.
Mkurugenzi wa ufundi wa ZFA Masoud Atai amesema, kwanza wanawapongeza waliomteua Morocco kwasababu wameona ni kocha mzuri na anaweza kuisaidia timu, lakini wao (ZFA) wamesema hawana tatizo na hilo na wamemruhusu kocha huyo akasaidiane na Mkwasa kuhakikisha timu inafanya vizuri na inapata matokeo mazuri.
“Morocco ni kocha mkuu wa Zanzibar Heros vilevile sasahivi ni kocha wa timu ya Mafunzo ambao ndio mabingwa wa Zanzibar na yeye ni mingoni mwa makocha wenye leseni A hapa Tanzania. Morocco ni kocha ambaye anafahamika na amewahi kuichukua Zanzibar Heros kwenye michuano mikubwa ya Challenge ambayo Zanzibar inashiriki”, amesema Atai.
“Ni kocha mwenye ‘experience’ sana ya mpira huu wa ukanda wetu wa Afrika Mashariki na ameshawahi pia kuzifundisha timu katika mashindano ya klabu bingwa Afrika Mashariki, ameshafundisha timu kombe la mataifa ya Afrika kwahiyo kwa kiasi anauzoefu wa juu sana. Tumeridhia na kuwapongeza wale ambao wamemteua kwasababu ya kazi hii ambayo sasahivi inatukabili”, alihitimisha.
Kamati ya utendaji ya TFF imemteua Mkwasa awe kocha wa Stars kwa muda na atasaidiwa na Morroco baada ya kamati hiyo kufanya kikao cha dharura siku ya Jumamosi na kumfuta kazi aliyekuwa kocha wa Stars Mart Nooij na kulivunja benchi zima la ufundi kufuatia ‘kisago’ cha goli 3-0 kutoka kwa Uganda ‘The Cranes’ kwenye mchezo wa kusaka tiketi ya kucheza CHAN uliopigwa visiwani Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment