Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
'Tambwe ni mfungaji bora wa Kombe la Kagame 2013, Ligi Kuu ya Burundi na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu uliopita.'
LICHA ya kufunga mabao 14 VPL msimu huu na mawili Kombe la Shirikisho barani Afrika mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope, amesema mshambuliaji Amissi Tambwe wa Yanga, hana uwezo mkubwa wa kufunga kwa jitihada zake binafsi.
Hanspope ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam akionesha kutojutia uamuzi wa klabu hiyo ya Msimbazi kumtema mkali huyo wa mabao.
Katika kutetea hoja yake hiyo, Hanspope amesema Tambwe hawezi kufunga mabao kwa juhudi zake binafsi, hivyo hana mchango wowote katika kikosi kama cha Simba ambacho kinahitaji wachezaji wenye uwezo wa kubadili matokeo kwa jitihada zao binafsi.
"Tambwe anafunga magoli ambayo ni 'expectable' (yanayoonekana hata kabla ya kufungwa). Hana uwezo kama (Emmanuel) Okwi wa kufunga kwa jitihada zake binafsi, tena katika mazingira yasiyotarajiwa," amesema Hanspope.
Kiongozi huyo wa Simba amesema Tambwe anafunga mabao kwa kutafuniwa na wachezaji wenzake.
Tambwe ambaye anaidai Simba mamilioni ya shilingi kutokana na kumtema dirisha dogo Desemba mwaka jana, ndiye mchezaji mwenye 'hat-trick' mbili VPL msimu huu, akishikilia rekodi yake ya msimu uliopita ambao pia aliondoka na mpira mara mbili dhidi ya Mgambo Shooting Stars na JKT Oljoro FC.
0 comments:
Post a Comment