RAMADHAN Singano ‘Messi’ aliifungia Simba goli moja katika
ushindi wa 2-1 dhidi ya Azam fc katika mechi ya ligi kuu soka Tanzania bara
iliyopigwa mwishoni mwa juma lililopita uwanja wa Taifa.
Goli lingine likifungwa na Ibrahim Hajib, huku bao la
kufutia machozi la Azam likifungwa na Mudathir Yahya.
Wakati wa kushangilia goli lake, Singano alivua jezi na
kuonesha fulana yake iliyoandikwa kwa maneno ya kiarabu yenye maana ya ‘Fadhila
au neema za Mwenye enzi Mungu zipo juu yangu’, Kwa mujibu wa mtaalamu mmoja wa
lugha ya kiaarabu aliyezungumza na MPENJA BLOG.
Alipofuatwa Singano mwenyewe alisema: “Mungu ndio kila kitu
kwangu, mimi ni Muislamu, naiheshimu dini yangu na mwenye enzi Mungu ndiye kila
kitu kwangu, fadhila zake ni kubwa kwangu ndio maana nimeendelea kucheza kwa
mafanikio ndani ya klabu yangu ya Simba”.
Singano ambaye ni muumini mzuri wa dini ya kiislamu na
wenzake wanamuita ‘ustadhi’ amefunga magoli matano msimu huu na amekuwa kwenye
kiwango bora kwa muda mrefu sasa.
Kuhusu ndoto za soka Singano anesema: “Nina malengo ya
kufika mbali kama Mungu akipenda, najituma na kuyalinda mazoezi na kiwango changu,
ipo siku milango itafunguka”.
0 comments:
Post a Comment