Kushoto ni mshambuliaji wa Platnum FC ya Zimbabwe Donald Ngoma akiwajibika.
UONGOZI wa Yanga ambao kwa sasa upo katika pilikapilika nyingi kujiandaa na pambano dhidi ya Etoile du Sahel ya Tunisia, umekubaliana na ushauri uliotolewa na kiungo wao fundi, Haruna Niyonzima juu ya kumsajili straika matata wa FC Platinum ya Zimbabwe.
Niyonzima mara baada ya kurejea kutoka Harare, Zimbabwe walipoenda kucheza mechi ya marudiano na Platinum katika Kombe la Shirikisho, alinukuliwa kuwa hakuna mtu aliyewasumbua uwanjani katika mechi hiyo waliyolala bao 1-0 kama Donald Ngoma na kutamani Yanga imsajili wacheze wote.
Viongozi wa Yanga wameufanyia kazi ushauri huo na sasa wanafanya kazi moja kubwa ya kuhakikisha inamnasa mshambuliaji huyo makini, msumbufu kwa mabeki zaidi ya Didier Kavumbagu waliyekuwa wakimpigia jaramba kumrudisha kikosini.
Mshambuliaji huyo mwenye nguvu amekubalika Yanga, uwezo wake umewachanganya mabosi wa Yanga akiwamo kocha Pluijm na wakaanza mchakato wa kumsajili.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka ndani ya Yanga zinasema tayari klabu hiyo imeshaanza mchakato wa kufanya mazungumzo ya kumalizana na raia huyo wa Zimbabwe ambaye ameonyesha kukubali kuja kufanya kazi chini ya makocha Mholanzi Hans Pluijm na mzalendo Charles Mkwasa.
Bosi mmoja wa Yanga amesema tayari wamefanikiwa kuweka sawa kila kitu na wakala wa Ngoma amewaita viongozi wa Jangwani kutua Zimbabwe kumaliza dili hilo na kama kila kitu kitakuwa sawa na akafanikiwa kusajiliwa, atazima jaribio la kurudishwa kwa Kavumbagu.
“Kuna mshambuliaji mmoja alivaa jezi namba 11 katika mchezo wetu wa marudiano dhidi ya Platinum anajua sana, hawakuja naye wakati tulipowafunga 5-1,”alisema bosi huyo.
“Tulifanya naye mazungumzo kule kidogo, lakini tuliporudi hapa tukafanikiwa kuongea na wakala wake amekubaliana na ofa yetu lakini wanataka twende kule tukamalize, tunajipanga.
“Mchezaji mwenyewe pia ameonekana kuvutiwa na timu yetu hasa juu ya kusonga mbele katika Kombe la Shirikisho, anaona ndiyo sehemu itakayomtangaza zaidi amekubali kuja ngoja tuone itakavyokuwa.”
Source: Mwanaspoti


0 comments:
Post a Comment