MPENJA BLOG kama ilivyo kwa Watanzania wengi inawatakia kila la kheri Dar Young Africans katika mechi yao ya kwanza ya hatua ya 16 bora ya kombe la Shirikisho dhidi ya Etoile du Sahel ya Tunisia inayopigwa leo kuanzia majira ya saa 10:00 jioni.
Yanga inahitaji hazina kubwa ya magoli ili kurahisisha kazi katika mechi ya marudiano itayopigwa wiki mbili zijazo nchini Tunisia.
Kwa wanaofuatilia soka la Uarabuni wanatambua fika kuwa hawa jamaa wanapenda sana kulazimisha mipango yao wanapokuwa ugenini na nyumbani.
Wakiwa ugenini wanacheza soka la polepole, ujanja mwingi wa kupoteza muda, kumlaumu mwamuzi na kujiangusha.
Lengo lao ni moja tu ambalo ni kumfanya mwenyeji achanganyikiwe na kuondoka mchezoni, na wakifanikiwa kwa hilo, basi wanakutoa wakifika kwao.
Dawa yao ni kutoiga wanachofanya wao, ukipata mpira wakimbize mchakamchaka na hakikisha kila unapomiliki mpira unasonga mbele kutengeneza mashambulizi.
Waarabu wakishafungwa hujitahidi angalau kufunguka, lakini bado wanakuwa na nidhamu ya uoga kukwepa kufungwa magoli mengi.
Yanga wanatakiwa kutambua wazi kuwa Etoile wamekuja kutafuta sare tu au ushindi lakini si kufungwa magoli mengi, halafu wakitegemea kumaliza kazi Tunisia.
Ushauri kwa Yanga ni kuhakikisha wanashambulia sana na kujilinda kwa nidhamu.
Mpira hauna adabu, unaweza kushambulia muda wote na kadiri unavyozidi kukaa eneo la mpinzani, akili inakufanya ulemae, unawaza muda wote kufunga na hapo ndipo unaona mabeki wote wanaanza kupanda kuongeza mashambulizi.
Ni kweli hakuna haja ya mabeki kukaa nyuma wakati timu ina mpira muda wote, lakini kuna kitu kinaitwa mashambulizi ya kushitukiza.
Wote mnaweza kupanda, lakini mkashitukizwa ka kufungwa goli la kizembe.
Yanga washambulie lakini wawe na nidhamu ya ulinzi.
Cha msingi dakika 15 za kwanza wahakikishe wanapata angalau goli moja au mawili na kama itatokea hivyo watawafanya Etoile wacheze kwa kufunguka kidogo na hapo ndipo Yanga wataweza kuwashambulia vizuri kwasababu watakuwa wanapungua nyuma.
Mashabiki wa soka watambue kuwa Yanga wanacheza na timu kongwe barani Afrika, wasifikirie kushinda tu, bahati mbaya katika mpira wa miguu kila timu ina haki ya kushinda.
Etoile kushinda ni haki yao pia, lakini faida ya nyumbani inatakiwa kuwabeba Yanga ingawa siku hizi mpira huu wa kisayansi haujali nyumbani wala ugenini, popote unaweza kumkandamiza mpinzani wako kama ukijipanga.
Mashabiki bila kujali unazi wa timu ishangilieni Yanga kwa dakika zote 90.
Kwa ubora kikosi cha Yanga, imani yetu ni kushinda tena kwa magoli mengi.
Hatuna shaka na uwezo wa kocha Hans van der Pluijm, ni mtu sahihi na anajua kusoma mazingira ya mechi na siku zote mipango yake inaisaudia Yanga
Ni hayo machache tu!....
Mungu ibariki Tanzania Mungu ibariki Yanga!

0 comments:
Post a Comment