NDANDA FC wametangaza vita kuelekea mechi zao mbili za
mwisho dhidi ya Kagera Sugar na Dar Young Africans.
Kesho kutwa Ndanda watachuana na Kagera Sugar uwanja wa
Nangwanga Sijaona na mei 9 mwaka huu katika uwanja huo huo watakabiliana na
mabingwa Yanga kufunga msimu wa 2014/2015.
Mpaka sasa Ndanda inashika mkia katika msimamo ikiwa na
pointi 25 baada ya kucheza mechi 24, sawa na Prisons wenye pointi 25 nafasi ya
12 wakicheza mechi 24, pia Polisi Moro wapo nafasi ya 13 kwa pointi 25 kufuatia
kushuka dimbani mara 25.
Kuelekea mechi ya jumamosi ambayo Ndanda lazima washinde
kama wanataka kubaki ligi kuu, afisa habari wa klabu hiyo, Idrissa Bandali
amesema kila mechi ya ligi kuu ni ngumu na wamejipanga kuvuna pointi sita
zilizobaki.
“Kila mechi ya ligi kuu ni ngumu, mechi ya Kagera sio
rahisi, lakini inategemea na maandalizi yako, tutaingia kwenye mechi zote
tukihitaji ushindi kuanzia ya Kagera na baadaye ya Yanga.” Amesema Bandali na
kuongeza: “Unajua mpira wa miguu ni mchezo wa dakika 90’, pia kusema timu
imeshuka msimu huu ni mpaka pale mechi za mwisho zitakapokamilika mei 9 mwaka huu. Hapo tutajua kama tunashuka
au tunabaki”.
Bandali ameongoza kuwa tayari bingwa ameshajulikana, lakini
nani anashuka ni mpaka tarehe 9.
“Tunataka kuondoa fikra za watu kuwa tunashuka, hatuwezi
kuondoa kwa maneno bali ni kwa ushindi, tunaingia uwanjani tukiwa na changamoto
kubwa, lakini tutafanya kwa vitendo”.
0 comments:
Post a Comment