Na Saleh Ally
JONAS Gerrard Mkude, mmoja wa viungo kinda kabisa hapa nchini ambaye ameonyesha njia kwamba anaweza
soka, akijiendeleza anaweza kufanya vizuri zaidi. Ukimtazama anaitumikia Simba, utakubaliana nami na wengi wameliona hilo.
Mkude amefanikiwa kuwafunika wageni kama Pierre Kwizera ambaye kwa mtazamo wangu, kamwe hakuwa mchezaji mbaya lakini ubora wa Mkude ulifanya Simba ione hana lolote na ikakubali kumuachia kiungo huyo raia wa Burundi aende zake anapopataka.
Watanzania nikiwemo mimi, tumekuwa tukililia Mkude apewe nafasi. Nimekuwa nikikasirishwa na makocha wa kigeni wanaoshindwa kumuamini.
Mmoja wa makocha hao ni Mart Nooij, raia wa Uholanzi, ambaye ameendelea kuteua kikosi chenye wakongwe rundo huku akijua Stars sasa haiko katika mashindano yoyote, hivyo ni bora kujenga kikosi cha chipukizi ambao watakuwa msaada baada ya mwaka mmoja ujao.
Kumtetea Mkude ni kutetea jambo moja kubwa ambalo Mtanzania yeyote mzalendo anapaswa kulifanya. Nalo ni kutetea taifa letu. Mkude ni kijana wa Kitanzania, pia kuitetea nchi yetu iwe na timu bora na kuachana na makocha wageni wanaotaka kutetea vibarua vyao bila ya kuangalia manufaa itakayopata Tanzania.
Wakati ninamtetea Mkude, ndiyo wakati huohuo ambao ninamkosoa bila haya hata kidogo, bila woga wala kuhofia lawama.
Tanzania inaharibikiwa na vitu vingi kwa kuwa watu wanahofia kulaumiwa. Watu wanataka kuonekana wazuri na waungwana sana katika jamii fulani, hata kama wanaona mambo yanaharibika.
Najua ukweli unauma, lakini leo nafikisha ujumbe sahihi ninaoamini utakwenda kwenye mirija ya damu ya moyo wa Mkude na kupitiliza kwenye ubongo wake kwa ajili ya kutafakari. Akiwa ‘fair’ atayafanyia kazi, akiwa si hivyo, atanuna, mwisho ataendelea kuharibikiwa na mimi nitaendelea kudunda kama kawaida, sitakosa chochote.
Nimekuwa nikishangazwa na tabia ya Mkude, mara kadhaa nikimkuta katika ‘kibaa’ kimoja eneo la Kijitonyama akipombeka. Wakati mwingine muda mchache kabla ya kwenda mazoezini au baada ya kutoka.
Nimekuwa nikimpita katika eneo hilo akiwa ameegesha gari lake aina ya Toyota GX 110 ambalo alipewa na uongozi wa Simba baada ya kusaini mkataba mpya. Usisahau pia alikomba Sh milioni 40. Baada ya mkataba wake mpya tuliwasifia Simba, kwamba wanatoa changamoto ya vijana wa Kitanzania kutamani kuwa kama Mkude.
Lakini sasa inaonekana tofauti kwa kuwa nimepewa hadithi nyingi za tabia za ulevi za Mkude. Hadithi yake ya kutafutwa usiku na baadhi ya viongozi, wakamkuta baa akiwa amelewa chakari. Akapelekwa Zanzibar huku akijitapikia.
Siku kadhaa zilizopita, Dawati la Championi lilifikishiwa malalamiko kwamba Mkude amekuwa akishinda mtaa fulani, pombe kwenda mbele, mabinti wakiwa pembeni.
Lengo langu si kumkorofisha Mkude, ingawa akiamua hivyo pia si shida kwa kuwa Watanzania wengi kukosolewa ni uadui. Nataka nimuambie kwa kasi ya mbwembwe na kufanya mambo ya ulimbukeni anayokwenda nayo, haitachukua muda atapotea.
Vijana wengi wanaitaka nafasi yake, sasa kuna mtu kama Abdi Banda ambaye anaonyesha kabisa ana ‘njaa’ ya mafanikio. Kama Mkude anaendelea hivyo, siku chache zijazo atapotea na mwisho atawaangushia lawama viongozi kwa kuwa tunajua huwa wanaharibu, itakuwa si rahisi kuamini kiungo huyo ana matatizo.
Nimekuwa nikifuatilia uchezaji wake kwa karibu sana. Mara kadhaa, nimeona mambo ambayo hayaniridhishi na hasa upotezaji wa pasi na upungufu wa nguvu ukilinganisha na ilivyozoeleka. Naamini hii inatokana na ukosefu wa muda wa kupumzika vya kutosha, utulivu wa kuwaza kazi na pia malengo au matamanio ya kufanya vizuri zaidi.
Kweli Mkude ana kipaji, lakini pombe na kutofuata utaratibu wa soka linataka nini, umewamaliza wengi na Mkude anaweza kuwa shahidi, sihitaji kuwataja majina kwa kuwa tupo nao mitaani.
Lazima Mkude abadilike, lazima ajue yeye si Mtanzania anayejua mpira kuliko wote. Kama anatamani kuwa kama mchezaji fulani wa Ulaya, lazima ajue mwenzake anajituma na anafuata vizuri misingi ya nini soka linataka.
Kama Mkude anaona gari alilonalo sasa ndiyo bora na kali kuliko yote, anajidanganya. Akijituma atapata mshahara au maslahi bora zaidi na itakuwa rahisi kupata gari bomba zaidi ya alilonalo.
Hakuna binadamu aliyewahi kujisifia pombe imemsaidia, labda kiwanda cha bia ambacho kinaingiza faida baada ya mauzo lakini si mtumiaji, kila mmoja analia na hasara tu au majuto mwishoni!
Lazima iwe sasa, huu ujumbe naufikisha kwako Mkude, ukibadilika, mambo yatakuwa poa na itaonekana, uking’ang’ania mlango wa maisha uliyoingia, utaona kitakachofuata, nacho ni aibu na utageuka mtu wa kulalamika tu.
SOURCE: CHAMPIONI


0 comments:
Post a Comment