Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
'Kumekuwa na tabia ya klabu za Ligi Kuu kugoma kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo vya viwanja mbalimbali nchini Tanzania kwa madai lukuki yakiwamo ya uchakavu wa vyumba husika na imani za kishirikina.'
MUDA mfupi baada ya TFF kuzipiga faini klabu mbalimbali nchini kwa kugoma kuingia viwanjani na utovu mwingine wa nidhamu, uongozi wa Ruvu Shooting Stars ya Pwani unahaha kuliomba shirikisho hilo la soka nchini kutoipiga faini kwa kutoingia vyumbani Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga jana.
Akizungumza na mtandao huu kwa simu akiwa Uwanja wa Ndege wa Mwanza leo asubuhi, Msemaji wa Ruvu Shooting Stars, Masau Bwire, ameiomba TFF kutoipiga faini ya Sh. 500,000 timu yake kwa kugoma kuingia kwenye vyumba hivyo vya kubadilishia nguo jana kwa madai kuwa vyumba hivyo si salama kwa afya.
"Hali ya vyumba vya wachezaji kwenye Uwanja wa CCM Kamabarage ni mbaya. Si kwamba sisi (Ruvu Shooting Stars) tunaamini ushirikina, la hasha, vyumba hivyo havifai kwa afya za binadamu. Mkiruhusu wachezaji wakae mle ndani kwa dakika 15, wote watahara," amedai Bwire.
Hata hivyo, alipoulizwa kama Kagera Sugar FC hawakuingia vyumbani jana katika mechi yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Bwire amekiri kuwa kikosi cha kocha mkuu, Jackson Mayanja, kiliingia vyumbani lakini akadai: "Wao ni wenyeji hapa, huenda wamezoea hali hiyo."
TFF imetangaza rasmi leo kuzipiga faini ya Sh. 800,000 klabu ya Simba na Sh. 500,000 klabu ya Mtibwa Sugar kwa kugoma kuingiza timu vyumbani kwenye Uwanja wa CCM Kambarage katika mechi zao dhidi ya Stand United FC na Kagera Sugar FC mjini Shinyanga.


0 comments:
Post a Comment