Na
Oswald Ngonyani
Kesho Jumamosi vinara wa VPL 2014/2015 Klabu ya soka
ya YANGA itamenyana na klabu
ya Etoile du Sahel katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam hiyo ikiwa ni baada ya
kuitoa Platinum ya Zimbabwe kwa jumla ya goli 5-2.
Baada ya kuivuka hatua hiyo, sasa Yanga
inaingia katika hatua ya 16 bora ikitaraji kupepetuana na moja ya klabu bora
kabisa barani Afrika, Etoile Du Sahel kutoka Tunisia na tayari wadau wa soka
wanajaribu kuiangalia mechi hiyo kwa jicho tofauti, wapo wanaoamini kuwa huo ndio
mwisho wa safari ya Yanga na wengine wakiamini historia mpya inaweza kuandikwa
kwenye mechi hiyo.
Wakati
wadau wengi wa mchezo wa soka nchini wakionekana kutofautiana kimtazamo kuhusu
mchezo huo, tayari Etoile du Sahel wametua nchini mishale ya Saa 10:10 za Alfajiri
kwa Ndege ya kukodi ya kampuni ya Nouvelair bj 4870 wakiwa na msafara wa watu
56 kwa ajili ya mchezo huo wa kwanza hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho
Afrika.
Msafara wa wapambanaji hawa umeongozwa na Makamu wa Rais wa
Shirikisho la Soka Tunisia (FTF), Krifa Jalel na wamekuja pia na Rais wa klabu
yao, Charefeddine Ridha, wachezaji 19, benchi la ufundi lenye watu 13,
Waandishi wa Habari 12 na wapenzi 10.
Baada ya kutoka ndani ya
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Etoile du Sahel
walipokewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro, na
kuelekea katika hoteli ya Ledger Plaza zamani Bahari Beach eneo la Kunduchi.
Kuelekea mchezo huo, mambo mengi sana
yanaweza yakazungumza na hata kupewa nafasi kubwa zaidi miongoni mwa mashabiki
wengi wa mchezo wa soka nchini Tanzania, lakini siku zote katika mchezo wa soka
lolote linaweza kutokea.
Nakumbuka kabla ya mchezo wa UEFA wa juzi
Jumatano baina ya klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani dhidi ya Porto ya Ureno
ni watu wachache mno walikuwa wanaipa nafasi Porto, lakini mwisho wa siku
Bayern akalala kwa goli 3-1 pale Estádio do Dragão.
Binafsi ninapingana na hisia za wanaomini kuwa
hiyo inaweza ikawa tamati ya wawakilishi pekee wa Tanzania kimataifa eti
kutokana na historia ya klabu hiyo kutoa fua dafu kila inapokutana na timu
kutoka Uarabuni.
Ni ukweli ulio wazi kuwa timu nyingi za
Tanzania zimekuwa ‘mdebwedo’ sana pale zinapocheza na waarabu lakini hii siyo
sababu moja kwa moja ya kuanza kuiengua Yanga katika mbio hizo za kuwania
ubingwa wa Kombe la shirikisho.
Ni kweli hakuna sehemu yoyote kwenye historia
ya klabu ya Yanga inayoonyesha kupata ushindi dhidi ya timu toka uarabuni zaidi
ya mwaka jana na hii inawafanya baadhi ya wachambuzi wa soka hapa nchini
kuamini huo ndio unaweza kuwa mwisho wa Yanga, kitu ambacho binafsi sitaki
kukipa nafasi kwani siku zote historia zipo kwa ajili ya kuvunjwa tu kwani hata
katika klabu kubwa za soka za Ulaya historia nyingine za miaka hata 70
iliyopita ndio zinavunjwa leo, hivyo huo unaweza kuwa mwanzo wa historia mpya
ya Vijana wa Jangwani kujenga historia iliyotukuka dhidi ya waarabu hao.
Tazama,
leo hii Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wamekuwa wakishindana katika mawanda ya uwekaji wa historia mpya za kufunga
mabao katika miaka hii na hata kufikia hatua ya kuzivunja rekodi za magwiji
wengine wa kandanda duniani akina Raul Gonzalez, Telmo Zara na Alfredo Di
Stefano wakiwemo.
Lakini pia tunaona jinsi akina Neymar na
Wayne Rooney wanavyozifukuzia kwa kasi ya ajabu rekodi za kufunga mabao za nchi
zao za magwiji kama vile Pele na Bobby Charlton. Kwa namna yoyote ile Washambuliaji
hawa wa kizazi kipya wanaweza kuvunja rekodi za magwiji hawa.
Yote kwa yote mifano iko mingi mno lakini
yote inatupeleka kwenye ukweli kwamba soka imebadilika na Yanga wana uwezo wa
sio kuifunga tu Etoile Du Sahel lakini pia kuitoa mashindanoni na hivyo kuweka
historia mpya kama ilivyofanya kwa Al Ahly msimu uliopita japo hatua ya matuta
iliwakwamisha safari yao hiyo.
Hata ukiangalia kwenye mechi dhidi ya Ah Ahly
Yanga ilikuwa na nafasi kubwa ya kuwatoa mabingwa hao wa zamani wa Afrika, kama
nyota wake Saidi Bahanunzi na baadaye Mbuyu Twite wangefunga mikwaju yao ya
penalti, lakini kwa bahati mbaya sana bahati haikuwa yao.
Nahodha Nadir Haroub’Cannavaro’ aliingia
kwenye historia na kuiweka klabu yake ya Yanga kwenye historia kwa kufunga bao
pekee lililoizamisha Al Ahly kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam ikiwa ni
zaidi ya miaka 28 baada ya Zamoyoni Mogella na Mtemi Ramadhani kuifungia Simba
mabao yaliyoizamisha timu hiyo kutoka Misri mwaka 1985.
Simba kama ilivyokuwa kwa Yanga nayo ilikuja
kutolewa Misri lakini iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania
kupata ushindi dhidi ya magwiji hao wa soka wa Afrika kwani ilikuwa ni kitu
kilichoonekana kutowezekana mbele ya fikra za watanzania wengi.
Tofauti yao na Yanga ni idadi ya mabao na
kiwanja kilichotumika kwani mwaka 1985 mechi hiyo ilipigwa kwenye dimba la CCM
Kirumba huku Yanga ikiifunga Al Ahly katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Kinachopaswa kufanyiwa kazi na YANGA ni
kujijengea imani kuwa hakuna linaloshindikana katika mchezo wa soka na kwamba
wana uwezo mkubwa tu wa kuifunga na kuitoa mashindanoni timu hiyo iwe kwa kufa
au kupona.
Klabu ya Yanga wala isitishwe na historia ya
Etoile Du Sahel, inapaswa kuingia uwanjani kucheza mpira, tena icheze mpira ule
ambao imekuwa ikiucheza katika siku za karibuni na hata kuwa tishio kwa vilabu
vingi vya VPL.
Sababu ya kushinda ipo wazi ndio maana hata
mashabiki na vibopa wa timu hiyo wameonekana kufungamana sana katika kipindi
hiki cha kuitakia heri timu yao ili iweze kufanya kitu ambacho wengi hawakipi
nafasi, kupata ushindi tena ushindi mnono.
Kama waliweza kuifunga Al Ahly ambayo ina
historia ndefu na kubwa zaidi kuliko timu hiyo kutoka Tunisia Yanga inaweza pia
sio kuifunga tu bali kuitoa mashindanoni Etoile Du Sahel.
Kikubwa ni kuamini kuwa wana uwezo huo lakini
lingine wasiweke malengo ya kuifunga tu timu hiyo bali kuitoa mashindanoni,
narudia tena wasiwaze tu kuifunga timu hiyo bali kuifungashia virago kunako
mashindano hayo makubwa.
Vijana hawa wa jangwani wanatakiwa kuitumia
vema faida ya kuanza nyumbani kwa kumaliza mechi mapema huku wakihakikisha kuwa
hawatoi mwanya kwa waarabu hao kufunga goli lolote lile, kwa kufanya hivyo
watajiweka katika mazingira yasiyo salama.
Ikumbukwe kuwa dhidi ya BDF ya Botswana Yanga
iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 nyumbani na kuvuka kwa faida ya bao la ugenini
kwani kwenye mechi ya marudiano ilifungwa mabao 2-1 na hivyo ikavuka kwa mabao
3-2.
Kadhalika kwenye mechi dhidi ya Platinum
Yanga iliifunga timu hiyo kutoka Zimbabwe kwa mabao 5-1 nyumbani kabla ya
kufungwa bao 1-0 ugenini na kuvuka kwa ushindi wa mabao 5-2.
Hapa utaona kwamba Yanga wanatumia vizuri
sana faida ya kuanza kucheza kwenye uwanja wake wa nyumbani na kumaliza mechi,
na ndivyo inavyopaswa kufanya kwenye mechi ya kesho ili kujiweka katika
mazingira salama.
Mimi ninaamini Yanga inao uwezo wa kuwatoa
Waarabu, Wewe Je!.
MUNGU IBARIKI DAR YOUNG AFICAN, MUNGU IBARIKI
TANZANIA
(0767 57 32 87)


0 comments:
Post a Comment