Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
'Mandawa ni mchezaji wa tatu kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara tangu ainzishwe msimu huu.'
ANAELEKEA kutimiza ahadi yake! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya straika hatari wa Kagera Sugar FC, Rashid Mandawa, kufikisha mabao 10 leo katika Ligi Kuu ya Bara msimu huu alipoifungia timu yake bao katika kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Simba SC Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.
Akiwa na mabao manne msimu huu na kutangazwa mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Bara wa Mwezi Novemba mwaka jana, Mandawa aliahidi kufanya kazi kwa bidii zaidi huku akiweka wazi ana nia ya kutwaa kiatu cha dhahabu cha mfungaji bora wa ligi hiyo msimu huu.
"Ninamshukuru Mungu kwa kuniwezesha kutwaa tuzo hii, ninawashukuru pia watendaji wote wa Kagera Sugar na mashabiki wetu kwa kuniunga mkono. Huu ni mwanzo mzuri kwangu msimu huu. Nitajitahidi nifanye vizuri zaidi, ikiwezekana kutwaa tuzo ya mfungaji bora.
"Mpaka sasa nina magoli manne ingawa watu wengi wanajua kwamba nina mabao matatu. Nilifunga dhidi ya JKT Ruvu, Polisi Moro, Coastal Union na Mtibwa Sugar. Ninawaahidi mashabiki wetu kwamba sitawaangusha," alisema Mandawa.
Goli lake la leo limemfanya amkamate mshambuliaji Mrundi Didier Kavumbagu wa Azam FC mwenye mabao 10 pia, moja nyuma ya kinara wa sasa Simon Msuva wa Yanga SC.
Je, Mandawa atafanya kweli na kutimiza ahadi yake katika mechi tano zilizobaki?


0 comments:
Post a Comment