MSHAMBULIAJI wa Yanga, Daniel ‘Danny’ Davis Mrwanda
amefichua siri kwamba yeye si mchezaji wa Yanga tu bali ni shabiki wa timu hiyo
toka enzi za utoto wake.
Mrwanda amefanya mahojiano maalumu na mtandao huu baada ya
kutwaa ubingwa wa ligi kuu kwa mara ya kwanza tangu aanze kucheza soka nchini.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba, Polisi Morogoro
amesema msimu wa 2009/2010 ambao Simba walichukua ubingwa bila kufungwa mechi
yoyote chini ya Patrick Phiri alitoa mchango mkubwa, lakini dakika za mwisho
akaondoka kwenda Vietnam kucheza soka la kulipwa hivyo hakuvaa medali siku
Simba wanakabidhiwa ubingwa.
Mwishoni wa juma lilipopita Yanga walitazwa mabingwa rasmi
baada ya kuifunga Polisi Moro magoli 4-1 na kufikisha pointi 55 amabazo
haziwezi kufikiwa na timu yoyote na wana mechi mbili mkononi dhidi ya Azam na
Ndanda fc.
MAHOJIANO YA MTANDAO HUU NA DANNY MRWANDA
Swali: Umesikiaje kuwa sehemu ya
mafanikio ya kutwaa ubingwa ndani ya klabu ya Yanga?
Mrwanda: Hakuna kitu kizuri kama kuona kitu ulichokuwa
unakitumikia kwa muda mrefu halafu kimefanikiwa, timu ya Yanga imetwaa ubingwa,
hii ni timu yangu, nimefurahi sana. Ni vigumu kujua nini mtu anawaza moyoni
mwake, lakini inafikia wakati inabidi uzungumze hisia za moyoni mwako, mimi
naipenda Yanga siku zote.
Swali: Ulianza kuipenda Yanga
ukiwa na umri gani?
Mrwanda: Katika maisha kuna vitu vinakuja bila kupanga,
siwezi kusema nilianza kuipenda Yanga nikiwa na umri gani, lakini naipenda sana
Yanga.
Swali: kitu gani kikubwa
kilikufanya uipende Yanga na si timu nyingine?
Mrwanda: Unajua si kitu nadharia, sisi tunakua katika
familia ambazo tayari kuna watu waliokutangulia, utakuta kuna wazazi au mtu
yeyote wa ‘kitaa’ anaizungumzia timu fulani na wewe mwenyewe unajikuta umeingia
moja kwa moja kwenye mfumo ule ule.
Swali: Mshambuliaji gani wa siku
za nyuma aliyewahi kuichezea Yanga na ukamkubali?
Mrwanda: Nilikuwa namkubali sana ‘Braza’ Lunyamila
(Edibily), alikuwa ananifurahisa sana, nilikuwa namfuatilia sana, ni mtu
aliyenivutia sana.
Swali:Kuna maneno ya mtaani
kwamba mchezaji huyu ni mpenzi wa timu fulani na anacheza chini ya kiwango
anapokutana na timu anayoipenda, wewe una mtazamo gani juu ya hilo?
Mrwanda: Mimi siwezi kumpinga mtu yoyote kuhusu hilo, ndio
maana nimewashukuru mashabiki, sio wote wanaofanya hivyo, wengi walikuwa
hawaamini kama mimi nipo pale kwa ajili ya kuitumikia timu moja kwa moja,
ukweli ni kwamba huu ni mpira, kuna wakati unashuka na kupanda, ni mambo ya
kimpira, unaona hata wachezaji wa ulaya kuna wakati wanapitia mazingira magumu,
lakini haimaanishi labda mtu haipendi timu fulani
Swali: Ni mara yako ya ngapi
kuvaa medali ya VPL hapa nchini?
Mrwanda: Itakuwa mara ya kwanza yangu japo katika timu
nilizopitia nilishawahi kusaidia timu ikapata ubingwa lakini dakika za mwisho
nikaondoka, mfano nilipokuwa Simba msimu wa 2009/2010 tukiwa na kocha Patrick
Phiri, tulichukua ubingwa bila kufungwa, lakini nikaondoka mwishoni mwa msimu
nikaenda Vietnam.
Swali: Ushindi huu unaupeleka kwa
nani?
Mrwanda: Naupelekea
kwa familia yangu, kwanza kwa mwanangu mdogo wa kike, ni jambo zuri, ni mwaka
ambao amezaliwa na tukio kubwa limetokea, ingawa niliwahi kuvaa medali nchi
nyingine nilizowahi kucheza, hapa nyumbani ndio mara yangu ya kwanza, najisikia
furaha sana.
0 comments:
Post a Comment