Na Mwandishi Wetu
KUNA viongozi wengi ambao naamini hawajui kuthamini vipaji au wachezaji muhimu katika timu zao.
Kutokana na kukosa weledi wa soka wanajikuta wanafanya mambo yasiyoeleweka kabisa.
Wakati wa dirisha dogo la usajili mwishoni mwa mwaka jana, Mwenyekiti wa kamati wa usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe alitangaza kuinasa saini ya beki wa kulia wa Mtibwa Sugar, Hassan Ramadhan Kessy.
Usajili huu haukuwa chaguo la kocha mkuu wa wakati huo, Patrick Phiri kwasababu wakati Kessy anawasili katika mazoezi ya Simba kwa mara ya kwanza uwanja wa Sigara, Chang'ombe, Dar es salaam, kocha huyo Mzambia alionekana kutomfahamu kabisa.
Phiri wakati anamtangaza Kessy kwa wenzake hakufahamu hata jina lake, akainama na kumuuliza kwa sauti iliyosikika, unaitwa nani? "Naitwa Hassan Kessy'.
Phiri akaendelea; "Leo tuna mchezaji mpya Kessy ambaye amesajiliwa, tufanye naye kazi vizuri na kuiendeleza Simba, karibu sana nani? oooh! Kessy".
Katika hali ya kawaida, hasa ukitumia mfano wa makocha wa nchi zilizoendelea kisoka, sio Ulaya tu hata baadhi ya mataifa ya Afrika, kocha ndiye mwenye jukumu la kutafuta wachezaji wa kuwasajili.
Leo hii Mourinho hawezi kuuliza mazoezini eti mchezaji aliyemsajili anaitwa nani? haiwezekani. Anamjua kwa kila kitu kwasababu yeye ndiye alimuona na kumpendekeza kwa wanaohusika kutoa pesa ya usajili.
Licha ya kumtomfahamu Kessy, Phiri alimuona mazoezini, alikiri mbele yangu simba ilipocheza mechi ya kirafiki na Mwadui fc mwaka jana kuwa "Kessy ni mchezaji wa ajabu, anacheza vizuri mno, hakika tumeongeza thamani kwenye timu".
Maneno haya yaliendana na ya mashabiki wengi waliombatiza jina la beki wa kulia wa Barcelona na Brazil, Danny Alves.
Baada ya Phiri kutimuliwa kufuatia kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Kagera, ingawa nyuma alikuwa na matokea ya sare sita na ushindi wa mechi moja, alikuja kocha Goran Kopunovic.
Kocha huyo Mserbia baada ya kumuona Kessy huko Zanzibar katika mechi ya kwanza ya kombe la Mapinduzi, Simba chini ya kocha msaidizi Seleman Matola ikifungwa 1-0 na Mtibwa Sugar, alikiri Kessy ni mchezaji mahiri.
Katika mechi tano alizoiongoza Simba mpaka kutwaa ubingwa, Kopunovic alimtumia Kessy kama beki wa kulia chaguo la kwanza.
Tangu Kessy atue Simba, beki mkongwe Masoud Nassor 'Cholo' amekuwa 'akichoma mahindi' kwenye benchi la Simba.
Mpaka sasa Kopunovic ameiongoza Simba katika mechi 12 za ligi, na katika mechi hizo, mechi moja tu ndiyo Kessy hakucheza.
Mechi hiyo ilikuwa dhidi ya Mbeya City fc januari 28 mwaka huu Simba ikilala 2-1. Sababu ya kutocheza ni kuwa na kadi tatu za njano.
Hajaishia kucheza tu mechi hizo, bali amekuwa akionesha kiwango cha juu mno. Kwasasa ndiye beki bora wa kulia wa Simba.
Kopunovic anamuamini sana, lakini viongozi wa Simba wamemuangusha.
Kessy hakika anamuliza Kopunovic, haamini kama hayupo kikosini. Siku akirudi atamushangilia kama alivyoshangilia baada ya Emmanuel Okwi kurejea mazoezini.
Katika kipindi muhimu, Kessy anasusia kuichezea Simba akiwa na madai ya msingi ambayo viongozi wanamzingua.
Wanamkata laki moja katika mshahara wake wa milioni 1 na nusu bila maelezo, hawajampa nyumba na garai kama matakwa ya mkataba yasemavyo. Pia hawajammalizia milioni 5 ikiwa ni sehemu ya ada yake ya usajili.
Kwa kipindi chote akiwa Simba, Kessy na umahiri wake anaishi nyumbani kwa akina Issa Rashid 'Baba Ubaya'. Haiwezekani!
Kwa jinsi alivyo lulu, Kessy ni mchezaji wa kumkumbatia, lakini viongozi wa Simba wanaleta Siasa.
Ni kutojua thamani ya mchezaji. Kessy ni mchezaji ambaye kila kocha anahitaji kuwa naye, Kopunovic anaumizwa sana na kukosekana kwa Kessy na hata sura yake inadhihirisha hilo akiwa mazoezini.
Anajua kuipandisha timu, kutengeneza mashambulizi, kupiga krosi na kurudi kukaba kwa haraka. Ushirikiano wake na Ramadhani Singano 'Messi' upande wa kulia umekuwa chachu ya mashambulizi mengi ya Simba.
Lakini leo hii kwasababu ya viongozi wa Simba, kocha anakosa huduma hiyo muhimu katika mfumo wake wa 4-3-3.
Mechi ya kesho na Kagera Sugar uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga, Kopunovic hatakuwa na beki wake kipenzi wa kulia.
Anaumiza kichwa namna atavyofanya, nadhani Cholo ndiye atamsaidia kwa kulazimisha.
Hakika inashangaza sana na kamwe Simba haiwezi kuendelea kwa aina hii ya viongozi. Kila jambo wanaleta siasa, ni waongo mno, mambo mengi wanadanganya umma lengo likiwa ni kujisafisha.
Inatakiwa wabadilike, watu wasileta ushabiki, Kessy ni mchezaji muhimu mno, ina faida zaidi kuzungumza naye kuliko kudanganya umma kuwa ameshindwa kuhudhuria mazoezi bila sababu.
Mchezaji huyo ameonesha kujitambua au ana washauri wazuri, hajababaishwa na jina la Simba, yeye anachotaka ni haki yake ya masilahi.
Simba zungumzeni na Kessy, Mlipeni haki zake, kocha afutwe machozi.


0 comments:
Post a Comment