Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
'Msuva alisema Jumatatu kuwa hana mpango wa kuihama Yanga kwa sasa.'
UONGOZI wa klabu ya Simba umesema bado haujakata tamaa ya kuiwania saini ya kinara wa mabao katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa sasa, winga Simon Msuva wa Yanga.
Licha ya Msuva kuweka wazi Jumatatu kwamba hana mpango wa kuihama Yanga kwa sasa, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope, amesema wanaisaka kwa udi na uvumba saini ya nyota huyo.
"Tunasubiri ligi imalizike Mei 9 ili tuanze majukumu yetu ya kuziba nafasi zinazopwaya Simba kwa sasa. Msuva bado yupo katika mipango yetu na tunamhitaji sana," amesema Hanspope katika mahojiano na moja ya vituo vya redio jijini hapa muda mfupi uliopita.
Msuva amekuwa akiwatoa udenda Simba kutokana na kukimbia kwa kasi, kupiga chenga na uwezo wake mkubwa katika kufunga mabao.
Mpaka sasa nyota huyo aliyekulia Azam FC kisha kuhamia Moro United kabla ya kutua Yanga 2012, amefunga mabao 17 VPL msimu huu akiongoza safu ya wafumania nyavu hatari akifuatwa na Amissi Tambwe wa Yanga pia mwenye mabao 14.
0 comments:
Post a Comment