NDANDA FC imebakiza mechi tatu kumaliza msimu huu wa ligi kuu soka Tanzania bara.
Mpaka sasa ipo nafasi ya 12 katika msimamo baada ya kucheza mechi 23 na kukusanya pointi 25.
Kitu kigumu kwa Ndanda ni kwamba imebakiza mechi mbili ngumu zaidi nyumbani na ugenini.
Mwishoni mwa wiki hii itacheza na Simba uwanja wa Taifa Dar es salaam.
Mechi ya kwanza uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara, Ndanda walifungwa 2-0 na Mnyama Simba na hii ilikuwa mechi ya kwanza kwa Simba tangu walipotoka kutwaa ubingwa wa kombe la Mapinduzi januari 13 mwaka huu uwanja wa Amaan Zanzibar kwa kuifunga Mtibwa Sugar kwa mikwaju ya penalti.
Mei 2 mwaka huu Ndanda wataikaribisha Kagera Sugar uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, hii ni mechi ya kufa na kupona kwa kikosi hicho cha Mtwara kuchele.
Mechi ya mwisho watacheza mei 9 mwaka huu dhidi ya Yanga uwanja wa Nangwanda Sijaona.
Hii ni mechi nyingine ngumu lakini kama Yanga watashinda mechi tatu kuanzia ya leo watakuwa tayari ni mabingwa wa ligi kuu.
Kocha mkuu wa Ndanda, Meja Mstaafu Abdul Mingange amesema licha ya kukabiliwa na mechi ngumu anapambana kuhakikisha jahazi halizami mikononi mwake.
"Tatizo langu kubwa lipo katika safu ya ushambuliaji, tunapata nafasi tunashindwa kuzitumia vizuri. Safu yangu ya ushambuliaji si butu sana lakini ni butu kwa kupata ushindi wa haraka tunavyotegemea", Amesema Mingange na kuongeza: "Tatizo si kufundisha tu, kama mchezaji anaweza kutengeneza nafasi halafu akashindwa kufunga nadhani sio kazi ya kocha tena, kocha naishia kufundisha namna ya mchezaji kutengeneza nafasi ili afunge, sio kazi kumwambia mchezaji tumbukiza mpira wavuni kama unavyojua kufunga ni kipaji na ndio maana wachezaji wachache ndio wafunga bora duniani"
"Katika juhudi zangu sitaki jahazi lizame mikononi mwangu, napambana, ningekuwa nimejua kuwa linazama mikononi mwangu ningekuwa nimetangaza kushindwa"
0 comments:
Post a Comment