| KIUNGO WA YANGA, SIMON MSUVA AKIPAMBANA NA WACHEZAJI WA ETOILE DU SAHEL KATIKA MECHI YA KOMBE LA SHIRIKISHO ILIYOMALIZIKA KWA SARE YA MABAO 1-1 KWENYE UWANJA WA TAIFA JIJINI DAR. |
Wawakilishi pekee katika michuano ya kimataifa timu ya Yanga SC, leo wamelazimishwa suluhu na Waarabu wa Tunisia Etoile Du Sahel mara baada ya kufungana bao 1-1 katika pambano la michuano ya shirikisho lililochezwa uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Yanga ndiyo waliokuwa wa kwanza kuandika bao kupitia kwa Nadir Haroub Ali 'Cannavaro' mnamo dakika ya pili tu kupitia mkwaju wa penati baada ya kiungo mshambuliaji machachari Simon Msuva kuangushwa katika eneo la hatari.
Baada ya kupata goli hilo ilikuwa ni kama Etoile wameamshwa usingizi kutokana na kuliandama lango la Yanga katika kipindi chote cha kwanza cha mchezo huku Yanga wao wakitegemea zaidi mashambulizi ya kushtukiza hasa kutokana na kuwa na washambuliaji wenye kasi kama Mrisho ngassa, Amissi Tambwe pamoja na Msuva Simon.
Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza pia kwa Waarabu hao kutoka Tunisia kuliandama lango la Yanga kama nyuki na kufanikiwa kusawazisha bao kupitia kwa mshambuliaji wao machachari Ben Amour Amine mnamo dakika ya 46 baada ya kupiga shuti kali la chini linalomshinda mlinda mlango wa Yanga Ally Mustapha 'Barthez' na kutinga moja kwa moja wavuni.
Etoile waliendelea kulishambulia lango la Yanga mara kwa mara huku Yanga wakiendelea kucheza kwa kujihami na kufanya mashambulizi ya kushtukiza.
Amissi Tambwe aliifungia Yanga bao la pili manamo dakika ya 83 lakini hata hivyo mwamuzi alikataa goli hilo kutokana na Tambwe kuwa ameotea.
Yanga walifanya mabadiliko mara tatu, wakiwatoa Nadir Haroub,Juma Abdul na Hassan Dilunga na nafasi zao kuchukuliwa na Saidi Juma Makapu, Rajab Zahir na Sherman.

0 comments:
Post a Comment