SARE ya 1-1 waliyopata Yanga dhidi ya Etoile du Sahel katika mechi ya kwanza ya 16 bora ya kombe la Shirikisho iliyopigwa uwanja wa Taifa Dar es salaam leo jioni imemfanya kocha Hans van der Pluijm awe na mzigo mzito katika mechi ya marudiano itayopigwa nchini Tunisia wiki mbili zijazo.
Yanga walikuwa wa kwanza kufunga goli katika dakika ya pili kupitia kwa Nahodha wake Nadir Haroub Ali 'Cannavaro' aliyefunga kwa mkwaju wa penalti baada ya winga Simon Msuva kuangushwa.
Kiukweli Yanga walianza mechi vizuri na kwa kasi kama ilivyo kawaida yao, lakini Etoile walionesha ukomavu mkubwa.
Yanga walifanya mashambulizi kadhaa baada ya kufunga goli, lakini Etoile wakaanza kucheza vizuri zaidi hususani safu ya kiungo na dhahiri pengo la Salum Telela lilionekana kwani Hassan Dilunga alishindwa kabisa kucheza katika kiwango chake.
Katika kipindi hicho ilibidi mlinda mlango Ally Mustapha Mtinge 'Bartez' afanye kazi ya ziada kuokoa michomo kadhaa langoni kwake.
Wakati Yanga ikihitaji ushindi, dakika za mwisho kipindi cha kwanza Cannavaro aliumia na hakurejea uwanjani kipindi cha pili na nafasi yake akachukua bwana mdogo Juma Said Makapu.
Pluijm akalazimika kumshusha Mbuyu Twite nafasi ya beki wa kati akicheza na Kelvin Yondani, huku Makapu akisogea mbele kidogo kucheza nafasi ya kiungo mkabaji.
Mapema kipindi hicho cha pili, Bedoui Rami alipiga shuti kali lililozama nyavuni baada ya kuona Bartez amekaa kizembe golini.
Goli hilo liliwatoa mchezoni Yanga na Etoile wakatawala mchezo.
Sasa Yanga wanahitaji sare ya kuanzia 2-2 ugenini au ushindi ili kusonga mbele.
Waarabu wana uzoefu na michuano ya kimataifa na huwa wanapenda kulazimisha matokeo wanayotaka.
Mtandao huu toka asubuhi uliwatahadharisha Yanga kuwa makini kulinda goli lao ili wasiwape mwanya Etoile kufunga goli la ugenini, lakini wameshindwa kufanya hivyo.
Soka huwa ni mchezo wa makosa, Yanga wamefanya makosa, lakini sio sababu ya kukata tamaa, bado wanaweza kupata matokeo ugenini japokuwa sio jambo rahisi kutokana na uimara wa Etoile.
Kinachotakiwa na kuamini wanaweza kushinda ugenini halafu wajiandae vizuri.
Yanga watulize akili, waangalie mapungufu yao na wanaweza kufanya kazi nzuri kama walivyofanya kwa Al Ahly ya Misri ambako walitolewa kwa mikwaju ya penalti.

0 comments:
Post a Comment