Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
'Uongozi wa Simba SC ulimsimamisha Chanongo kwa madai ya utovu wa nidhamu kabla winga huyo hajasajiliwa na Stand United FC kwa mkopo.'
BAADA ya beki mahiri wa pembeni kulia wa Simba SC, Hassan Kessy, kuikacha timu yake hiyo kutokana na kutotimiziwa matakwa ya kimkataba, winga Haroun Chanongo, naye amewasilisha madai katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) dhidi ya klabu hiyo ya Msimbazi, imefahamika.
Wakati kikosi cha mabingwa hao mara 18 wa Tanzania Bara kiko usukumani mjini Shinyanga kwa ajili ya mechi ya kesho ya Ligi Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar FC, Kessy hajafuatana nacho kutokana na kutolipwa sehemu ya malipo ya kusaini mkataba na kupewa nyumba ya kuishi.
Uchunguzi wa mtandao huu umebaini kuwa Chanongo ambaye yuko mbioni kutimikia DRC kufanya majaribio katika klabu ya TP Mazembe, amewasilisha barua TFF akitaka shirikisho limsaidie kupata stahiki zake Simba SC.
Miongoni mwa madai ya Chanongo dhidi ya Simba SC ni kulipwa pesa za mshahara ambazo klabu hiyo amedai klabu hiyo haijawahi kumlipa mshahara tangu ajiunge na Stand United FC Desemba mwaka jana.
Uchunguzi wetu umezama zaidi na kubaini kuwa mkataba wa Chanongo na Stand una kipengele kinachotamka wazi kwamba Simba SC inatakiwa kumlipa nusu ya mshahara na Stand inamlipa nusu nyingine, lakini tangu atue usukumani, hajawahi kupokea mshahara kutoka Simba SC.
Taariza za kina kutoka kwa mmoja wa mameneja wa Chanongo, zimeeleza kuwa winga huyo hajasaini mkataba mpya wa kuendelea kubaki Stand United FC kama ilivyodaiwa hivi karibuni na baadhi ya vyombo vya habari.


0 comments:
Post a Comment