Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
CHAMA la Wana, timu ya Stand United imefanikiwa kulinda bao lake la jana na kuongeza jingine leo asubuhi katika kujihakikishia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar FC Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.
Baada ya kuichapa Simba SC bao 1-0 Jumapili ya wiki iliyopita, timu hiyo inayonolewa na Mganda Mathias Lule ilipata bao dakika ya 43 jana jioni kwa penalti kupitia kwa mshambuliaji Mnigeria Abasalim Chidiabele ambaye pia ndiye alifunga bao lao la ushindi dhidi ya Simba SC.
Mechi hiyo iliahirishwa dakika ya 80 na refa Hashim Abdallah kutoka Dar es Salaam baada ya kunyesha mvua kubwa usukumani mjini Shinyanga kiasi cha kuwa kiza uwanjani.
Katika kumalizia dakika 10 za mchezo huo leo kuanzia saa 2:30 asubuhi, Stand iliongeza bao la pili dakika ya nne na ya 84 ya mchezo wote kupitai kwa Mnigeria huyo huyo alipowatoka mabeki na kufumua shuti kali.
Kocha Mkuu wa Kagera Sugar FC, Mganda Jackson Mayanja, ameuambia mtandao huu kwa simu kuwa: "Ilikuwa imepangwa tangu sisi tupoteze mechi. Marefa wameibeba wazi wazi Stand kwa sababu goli la pili la leo mfungaji alikuwa ameotea."
"Mashabiki waliokuwa wamefurika uwanjani hawakukubaliana na maamuzi hayo ndiyo maana wakaanza kurusha chupa za maji uwanjani hadi pale polisi walipoingilia kati," ameongeza kocha huyo.
Mayanja amesema kikosi chake tayari kiko njiani kutoka mjini Shinyanga kwenda jijini Tanga kumenyana na Coastal Union ambao jana walishinda 1-0 dhidi ya timu ya jiji moja ya Mgambo Shooting Stars kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Matokeo mengine ya mechi za jana ni Simba SC 5-0 Tanzania Prisons (Uwanja wa Taifa) na Mbeya City FC 1-1 Ruvu Shooting Stars (Uwanja wa Sokoine).
0 comments:
Post a Comment