
Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Joseph Omog, kocha mkuu wa Azam FC, amesema nidhamu na kutohamanika (kutopaniki) ndiyo kutaikoa timu yake kupoteza mechi yao ya marudiano dhidi ya El-Merrikh mjini Khartoum, Sudan wiki ijayo.
Azam itakuwa na kibarua kigumu ugenini mbele ya mabingwa hao mara 19 wa Ligi Kuu ya Sudan watakaporudiana katika mechi ya hatua ya awali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika mwishoni mwa wiki ijayo.
Mara tu baada ya Azam kuichapa El-Merrikh mabao 2-0 Uwanja wa Azam jijini jana, Omog alisema: "Bado tuna tatizo katika umaliziaji, tulifunga mabao matano katika mechi ya Ligi Kuu iliyopita dhidi ya Mtibwa Sugar na leo (juzi) tumefunga mawili."
"Bado tuna tatizo katika kumalizia nafasi nyingi ambazo tunazitengeneza. Ili kusonga mbele katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, tunapaswa kuwa na nidhamu ya hali ya juu katika kuwadhibiti wapinzani wetu nyumbani," alisema zaidi Mcameroon huyo.
Mabao ya Azam FC jana yalifungwa na kinara wa kufumania nyavu Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, Mrundi Didier Kavumbagu na mtokeabenchini John Bocco 'Adebayor'.
Ushindi huo ulikuwa kisasi baada ya Wasudan hao kuing'oa Azam FC kwa matuta katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Kagame jijini Kigali, Rwanda mwaka jana.

0 comments:
Post a Comment