Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Kikosi kilichokusanya pointi 11 katika mechi 13 zilizopita cha Tanzania Prisons FC kimetamba kitazinduka kwa kuichapa Yanga SC katika mechi yao ya kesho jijini Mbeya.
Prisons ambayo ililazimika kushinda mechi yake ya mwisho ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita dhidi ya Ashanti United na kunusurika kuporomoka daraja, itakuwa kibarua kigumu mbele ya Yanga SC wanaotaka kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, timu hizo zitakapocheza Uwanja wa Sokoine jijini humo kesho jioni.
Akiwa jijini Mbeya leo, Kocha Mkuu wa Prisons, David Mwamwaja ameuambia mtandao huu kuwa 'bunduki; zake ziko tayari kukiangamiza kikosi cha mabingwa hao mara 24, huku akiweka wazi kwamba wamelazimishwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kucheza mechi hiyo.
Mwamaja amesema kikosi chake kilichokuwa kimeweka kambi jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi ya mwishoni mwa wiki dhidi ya mabingwa watetezi Azam FC, kimelazimika kurejea jijini Mbeya baada ya kulazimishwa kucheza dhidi ya Yanga SC katikati ya wiki.
“Timu ilikuwa Dar es Salaam tukijiandaa kwa mechi dhidi ya Azam, lakini tumelazimishwa kurejea Mbeya kucheza dhidi ya Yanga," amesema kocha huyo wa zamani wa Simba.
Mechi ya Prisons dhidi ya Yanga ni ya raundi ya 15 ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ambayo ilipaswa kuchezwa mwishoni mwa wiki iliyopita, lakini ikapigwa kalenda na TFF kutokana na ushiriki wa Yanga SC katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mwaka huu.
'WATOTO WATAINYANYASA YANGA SC'
Mwamaja amesema kuwa katika kuhakikisha anawapa changamoto kubwa Yanga SC katika mechi ya kesho, atatumia wachezaji wengi wenye umri mdogo.
"Yanga SC tunawajua na wao pia wanajua moto wetu. Tumekuwa na matokeo ya sare nyingi, lakini sare si mbaya, bunduki zetu ziko sawa kwa ajili ya mechi hiyo. Ninaamini tutafanya vizuri hapa nyumbani tukitumia wachezaji wetu wengi vijana kutoka Kikosi B cha U20," amesema zaidi Mwamaja.
Prisons FC ina winga hatari wa kulia Hamis Maingo ambaye aliisawazishia katika mechi yao ya mzunguko wa kwanza ya sare ya 1-1 dhidi ya Simba SC Uwanja wa Sokoine Oktoba 25, mwaka jana.
Timu hiyo pia ina mabeki mahiri Nurdin Chona, ambaye anatajwa kuwa 'kiboko' ya mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, Mrundi Amisi Tambwe, na beki wa kulia Salum Kimenya ambaye amekuwa akishirikiana vyema na winga Maingo.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro ameuambia mtandao huu akiwa Mbeya leo mchana kuwa: "Tupo hapa Mbeya kwa malengo mawili; kwanza kuchukua pointi sita katika mecho zote mbili dhidi ya Prisons inayoshika mkia katika msimamo wa ligi na Mbeya City. Pili, kufanya maandalizi ya mechi yetu ya marudiano dhidi ya BDF XI FC mjini Gaborone, Botswana wiki ijayo."
Prisons FC ambayo ilifungwa na Yanga SC mabao 2-1 katika mechi yao ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu Uwanja wa Taifa jijini hapa Septemba 28, imeambulia sare katika mechi zote nne zilizopita, tatu ikicheza nyumbani dhidi ya City, Kagera Sugar FC na Ruvu Shooting Stars.
Timu hiyo iko hatarini kuporomoka kwani inashika mkia ikiwa timu pekee iliyokusanya pointi chache zaidi katika ligi hiyo msimu huu, pointi 11 kama ilivyodokezwa awali.
0 comments:
Post a Comment