
Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Kikosi cha nyota 22 wa Simba SC kimeondoka jijini hapa leo asubuhi kwenda mjini Shinyanga kuifuata Stand United FC, huku Kocha Mkuu Goran Kopunovic akitamba kufanya kweli dhidi ya timu hiyo ya usukumani.
Simba SC, ambayo ilishinda 2-0 dhidi ya Polisi Moro mjini Morogoro Jumapili, itakuwa na kibarua kigumu mbele ya Stand United FC watakapokutana Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga katika mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara Jumapili.
Humphrey Nyasio, msemaji wa Simba, ameuambia mtandao huu jijini hapa leo kuwa Goran ameahidi kushinda mechi hiyo ya Kanda ya Ziwa ili kujiweka pazuri katika msimamo wa ligi.
"Timu imeondoka leo asubuhi ikiwa na wachezaji 22. Tunajua itakuwa mechi ngumu kwetu, lakini kocha (Goran) ametuahidi tutashinda," amesema Nyasio.
Stand United FC, timu mpya VPL iliyokumbwa na migogoro ya kiungozi huku baadhi ya wachezaji na watendaji wa benchi la ufundi wakisimamishwa jana, iliitoka sare ya 1-1 na Simba Sc mzunguko wa kwanza kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Oktoba 4, mwaka jana,
Timu hiyo pekee ya Shinyanga Ligi Kuu, ilishinda 4-1 nyumbani dhidi ya Mgambo Shooting Stars Jumamosi.
Simba SC, iliyoshinda mechi mbili ugenini msimu huu ikishinda pia mbili na kupoteza mbili nyumbani, iko nafasi ya nne katika msimamo wa VPL ikiwa na pointi 20, tano mbele ya Stand United FC ambao wako nafasi ya 12 katika ligi hiyo yenye timu 14.
0 comments:
Post a Comment