Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Aliyekuwa kocha mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic anatarajiwa kutua Kenya kesho kuanza kazi rasmi ya kuinoa timu yake mpya ya AFC Leopards.
Ijumaa, Leopards walithibitisha kumteua Mcroatia huyo kuwa kocha mkuu wa timu yao akirithi mikoba ya Pieter De Jongh, raia wa Uholanzi ambaye amefukuzwa na klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL).
Ingwe kupitia kwa Katibu wake Timothy Lilumbi imethibitisha kuwa Logarusic, maarufu Loga anatua nchini humo kesho, Jumatano na kuanza kazi rasmi kwa kuiongoza Ingwe katika michuano ya timu 12 ya ubingwa wa Kenya kabla ya kuanza kwa ujao wa KPL.
"Tunatarajia kumpokea Loga kesho asubuhi. Tulishamtumia tiketi ya ndege. Ataanza kutekeleza majukumu ya timu mara tu baada ya kuwasili," amesema.
Loga (53) amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuinoa klabu hiyo ukiwa na sharti la kuifanya timu hiyo ingare kwa kushinda mechi nyingi zaidi katika kipindi hicho.
Mcroatia huyo alitua kwa mara ya kwanza Kenya 2012 akiipa mafanikio makubwa Gor Mahia. Amekaa bila timu tangu Agosti 2014 alipofukuzwa na uongozi mpya wa Simba, chini ya Rais Evans Aveva kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutokana na utovu wa nidhamu.
Akiwa Tanzania, Loga alidaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na baadhi ya wasanii wa filamu nchini, jambo ambalo lilidaiwa kuuchefua wanamsimbazi.

0 comments:
Post a Comment