Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
WANANDINGA 20 wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa
Stars wanaondoka kesho alfajiri kwenda mjini Bujumbura nchini Burundi tayari
kwa mechi ya kimataifa ya Kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya nchi hiyo
itayochezwa septemba 7 mwaka huu (jumapili).
Mholanzi, Mart Nooij, kocha mkuu wa Stars
amewaambia waandishi wa habari leo hii kuwa amekiandaa vizuri kikosi chake na
kina matarajiao makubwa ya kulipa kisasi cha kufungwa mabao 3-0 na Burundi Aprili
26 mwaka huu katika mechi maalumu ya kuadhimisha miaka 50 ya Muungano.
Katika mechi hiyo iliyopigwa uwanja wa Taifa
jijini Dar es salaam, Stars iliyosheheni wachezaji waliotoka katika mpango
maalumu wa maboresho ya Taifa Stars uliofanywa na shirikisho la soka Tanzania,
TFF, ilishindwa kuhimili makali ya
washambuliaji wa Burundi kama vile Didier Kavumbagu na Amiss Tambwe.
“Natambua Burundi ina wachezaji wazuri kama
Tambwe, Kwizera na Kavumbagu, lakini kwa kikosi tunachokwenda nacho tuna uhakika
wa kufanya vizuri na kulipa kisasi kwani Burundi walitufunga nyumbani.” Alisema
Nooij.
Nooij alisema kuwa wachezaji John Bocco, Aggrey
Morris na Aishi Manula wameachwa katika msafara wa Taifa Stars kutokana sababu mbalimbali.
Morris na Bocco ni majeruhi wakati Manula ameachwa
kwasababu tayari Nooij ana makipa wawili, Mwadini Ali na Deogratius Munish ‘Dida’,
hivyo hakuna sababu ya kwenda na kipa huyo kinda.
Nooij aliwataja wachezaji watakokweda Bujumburu kuwa
ni makipa Mwadini Ali (Azam fc) na Deogratius Munishi ‘Dida’, (Yanga).
Wachezaji wengine ni Shomari Kapombe (Azam fc), Oscar
Joshua (Yanga), Said Mourad (Azam fc), Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Yanga), Kelvin
Yondani (Yanga), Joram Mgeveke (Simba).
Wengine ni Saimon Msuva (Yanga), Erasto Nyoni
(Azam fc), Himid Mao (Azam fc), Amri Kiemba (Simba), Haroun Chanongo (Simba),
Salum Abubakary ‘Sure Boy’ (Azam fc), Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya, Qatar),
Hamis Mcha ‘Vialli’ (Azam fc), Juma Luizio (Zesco United, Zambia), Mrisho Ngasa
(Yanga), Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu (wote TP Mazembe, DR Congo).

0 comments:
Post a Comment