
Mshambuliaji wa Simba, Mkenya, Paul Kiongera amewatandika magoli mawili ndugu zake Gor Mahia, Mnyama akishinda 3-0 jioni.
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
WEKUNDU wa Msimbazi Simba wamefanikiwa
kuwatungua mabao 3-0 mabingwa wa ligi kuu nchini Kenya (KPL), Gor Mahia katika mchezo wa kimataifa wa
kirafiki uliomalizika jioni hii ndani ya dimba la Taifa jijini Dar es salaam.
Bao la kwanza la Simba lilifungwa
katika dakika ya 55 kipindi cha pili na mshambuliaji mpya kutoka Kenya, Paul
Kiongera baada ya kumalizia pasi murua iliyochongwa na Mganda, Emmanuel Anord
Okwi.
Okwi aliendelea kufanya vitu vyake
ambapo katika dakika ya 73 alipiga shuti kali lililotemwa na kipa wa Gor Mahia,
Patrick Odhiambo na mpira kumkuta Ramadhan Singano ‘Messi’ aliyefanya kweli na
kuzamisha mpira nyavuni na kuandika bao la pili.
Simba waliendelea kuonesha kiwango
kizuri na kulisaka lango la Gor Mahia na katika dakika ya 77 waliandika bao la
tatu kupitia kwa Paul Kiongera.
Baada ya kufungwa kwa bao la tatu
baadhi ya mashabiki wanaokalia jukwaa la kusini mwa uwanja wa Taifa na waliokuwa wanaishangalia Gor Mahia walianza
kuondoka uwanjani.

Hii unaweza kuitafsiri kuwa waliduwazwa
na kiwango cha Mnyama aliyeonekana kuwa na makali katika mchezo wa kwanza wa kimataifa
wa kirafiki tangu arejea kocha Phiri.
Okwi ambaye usajili wake bado
unaonekana kuwa na utata kwasababu timu yake ya zamani ya Yanga inadai ina
mkataba aliitwa benchi na Phiri katika dakika ya 79 na alipewa mkono wa pongezi kwa kazi nzuri,
huku mashabiki wa Simba wakishangilia kwa nguvu.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na
mwamuzi wa kati, Mathew Akrama kutoka mwanza, mashabiki wa Simba waliofurika
uwanjani walikuwa na amsha amsha za muda mrefu kutokana na kandanda lililokuwa
likitandazwa na vijana wa Patrick Phiri.


Okwi akifanya vitu vyake. (Picha na kamanda wa matukio)
Mashabiki hawakujaa uwanjani, lakini walitosha kwa mechi kama hii ya kirafiki na sababu kubwa ni namna klabu ya Simba ilivyozidi kuimarika chini ya Mzambia Phiri.
Mashabiki hawakujaa uwanjani, lakini walitosha kwa mechi kama hii ya kirafiki na sababu kubwa ni namna klabu ya Simba ilivyozidi kuimarika chini ya Mzambia Phiri.
Kiufundi Simba wameonekana kubadilika
kiuchezaji wakiwa na kasi nzuri, pasi za uhakika na mbinu za kutosha kulifikia
lango la mpinzani.
Wakiwa katika kambi ya Zanzibar, Phiri
alitumia muda mwingi kuwafundisha wachezaji wake namna ya kukaba kwa usahihi,
kupiga pasi za uhakika, kumiliki mpira na kushambulia kwa nguvu.
Mbinu sahihi za Phiri katika mambo haya
muhimu yamewafaidisha Simba na wameonekana kucheza mpira wa kufundishika na
kupiga mabao matatu kama waliyofungwa na Zesco United katika mechi ya Tamasha
la Simba, Agosti 9 mwaka huu katika uwanja huo huo.
Ramadhani Singano ‘Messi’, Paul
Kiongera, Okwi, Uhuru, Juma Awadh walionekana kuonana vizuri uwanjani na hata
Shaaban Kisiga alicheza soka la kuvutia.
0 comments:
Post a Comment