Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
WEKUNDU wa Msimbazi, Simba, jumamosi ya wiki hii watakabiliana
na timu mpya ya ligi kuu soka Tanzania bara, Ndanda FC katika mchezo wa pasha pasha kuelekea ligi kuu
ndani ya dimba la Nangwanda Sijaona Mkoani Mtwara.
Simba Walioitandika Gor Mahia mabao 3-0 jana
uwanja wa Taifa katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki watasafiri kuelekea
Mtwara ijumaa ya wiki hii tayari kwa kuwafuata wapinzani wao waliotamba kuwafunga
wakali hao wa Msimbazi.
Mabao ya Simba jana yalifungwa na Mkenya, Paul
Kiongera aliyetungua mawili na moja likafungwa na Ramadhani Singano ‘Messi’.
Baada ya mechi ya Mtwara, Mnyama atarejea Dar es
salaam kuendelea na programu ya mazoezi kujiandaa na mchezo wa ufunguzi wa ligi
kuu bara dhidi ya Coastal Union, Septemba 21 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini
Dar es salaam.
Wachezaji wote wa Simba leo walipewa mapumziko na
kocha mkuu Patrick Phiri na kesho wataanza mazoezi katika uwanja wa Boko
Veterani, jijini Dar es salaam.
Badala ya kurejea Zanzibar baada ya mechi ya Gor
Mahia, kama ilivyoelezwa awali na makamu
wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, vijana wa Patrick Phiri wanaingia
kambini kesho katika Hoteli ya Shynovo, maeneo ya Africana, Mbezi, Beach, Dar
es salaam tayari kwa mawindo ya ligi kuu.
Kabla ya kambi inayoanza kesho, Simba ilijichimbia
Zanzibar ambako ilicheza mechi tatu za kirafiki na kushinda zote.
Ilianza kwa kuichapa Kilimani City mabao 2-1, halafu
ikaitandika Mafunzo 2-0 na kumalizana na KMKM kwa kutoa kipigo cha mabao 5-0,
mechi zote zilipigwa Zanzibar.
Mechi ya jana ilikuwa ya kwanza ya kimataifa ya
kirafiki tangu kurejea kwa kocha Mzambia, Patrick Phiri.
Simba ilicheza vizuri katika mechi hiyo na kukonga
nyoyo za mashabiki na viongozi wa kalbu hiyo.
Wachezaji wa Simba walitandaza soka chini,
wakapiga pasi za uhakika na kushambulia kwa mipango na kuibuka na ushindi mnono
dhidi ya mabingwa wa Kenya.
0 comments:
Post a Comment