
Atachomoka kwa hili?: Usajili wa Emmanuel Okwi umegubikwa na utata mzito
Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
Bado kuna ‘ giza ‘ katika usajili wa mshambulizi,
Emmanuel Okwi kutoka timu ya Yanga SC na kujiunga na Simba SC, lakini nyuma
yake tayari kuna baadhi ya malamiko ya msingi ambayo baadhi ya timu wamepeleka
katika ‘ Kamati ya nidhamu ya TFF’ kwa sababu za kukiukwa kwa kanuni, sheria na
taratibu za uhamisho wa wachezaji.
Kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili, kiongozi
mmoja wa klabu kubwa nchini alimfuata mchezaji, Salim Mbonde wa klabu ya Mtibwa
Sugar na kumwambia ‘ tunataka kukusajili’. Mbonde mchezaji chipukizi wa Mtibwa
alimjibu kiongozi huyo kuwa; ‘ Bado nina mkataba wa miaka miwili na timu yangu’. Yalikuwa ni
majibu ya hekima na busara kutoka kwa mchezaji huyo.
Siku zote ni makosa mchezaji kuzungumza mambo ya
usajili na timu nyingine kabla ya klabu kufahamu kwanza. Mchezaji alitambua
hilo lakini ajabu kiongozi huyo ambaye yupo pia katika kamati nne za Shirikisho
la soka nchini, huku akihodhi pia nafasi ya ungozi wa juu katika klabu yake na
chama cha soka ni wazi hakuwa akifahamu lolote kuhusiana na anachotakiwa
kufanya.

Usajili wa Abdi Banda kutoka Costal Union kwenda Simba sc una utata pia.
Licha ya kujibiwa hivyo, bado kiongozi huyo
aliendelea kumshawishi mchezaji huyo na kumwambia ‘ Nenda kavunje mkataba kwa
Jamal Bayser ( kiongozi wa Mtibwa Sugar) tutakuja kukusajili’. Je, unategemea
nini kutoka kwa kiongozi wa namna hii hasa wakati ambao anatakiwa kuvaa uhusika
wa nafasi yake kama mmoja wa wajumbe wa Kamati ya utendaji wa TFF?.
Ukiona wachezaji wanasajiliwa bila ya kufuatwa kwa
taratibu tambua nyuma yake kuna nguvu ambayo huwafanya kukubali japo ni makosa
ambayo yapo wazi katika kanuni za usajili. Itakuwa ni kuendelea kupoteza imani
endapo wachezaji kama Emmanuel Okwi, Abdi Banda, na Shaffih Hassan wataruhusiwa kucheza mpira msimu ujao
kutokana na makosa waliyofanya. Okwi bado ana mkataba na Yanga kama ambavyo
mwenyekiti wa klabu hiyo alivyowahi kusema, Banda bado ana mkataba wa miaka
miwili na Coastal Union wakati Shaffih alisaini mkataba wa muda mrefu na klabu
ya Ashanti United mwishoni mwa mwaka uliopita.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi anatakiwa kuachana na maamuzi ya busara badala yake kanuni na sheria zitumike
Wachezaji hawa wote watatu wana mikataba na klabu
mbili kwa wakati mmoja. Ni wapi imewahi kufanyika jambo kama hilo? Ni Tanzania
tu huku watu wanaofanya hivyo wakiwa ni viongozi wa juu wa mpira ngazi ya
Taifa. Kama kweli ipo nia ya dhati ya kukomesha vitendo hivyo, basi ni kuanza
kuchukua hatua kwa viongozi wa klabu ambao wanakwenda kuwashashi wachezaji wa
timu nyingine kuvunja mikataba na klabu zao hili tu wapate urahisi wa kuwapata
wachezaji hao.
Mchezaji anaweza kucheza mahali kokote endapo
hakutakuwa na tatizo linalomzuia, ndiyo maana klabu kubwa dunia zinafanya
biashara ya kuuziana wachezaji badaa ya viongozi wa timu hizo kukutana na
kukubaliana.
Real Madrid ni mfano bora, ni klabu kubwa na yenye
mafanikio barani ulaya, tazama walichofanya msimu huu uliopita wa usajili. Ton
Kroos alisajiliwa na timu hiyo kutoka klabu bingwa ya UJerumani Bayern Munich,
wakati huo huo kiungo Xabi Alonso akitoka kwa mabingwa hao na kujiunga na
Munich, si hao tu vipi kwa biashara yao na Manchester United? Imekwenda safi na
mahusiano yao yanaendelea kukua tangu wakati ule wa kina David Beckham,
CrIstiano Ronaldo na sasa kina Angel Di Maria na Javier Hernandez.
United pia imekuwa na mahusiano mazuri na klabu ya
Sporting Lisbon ya Ureno lakini uzuri huo hauji kwa kuvunjwa kanuni na sheria
za usajili zaidi ya kuzilinda kwa manufaa ya mpira wa miguuu. Okwi
haishindikani kutoka Yanga lakini unaweza kujiuliza Yanga ni wajinga hadi
wamng’ang;anie?. Je, Coastal wamekosea kumfungia Banda, ni maswali ambayo
hayatakiwi kwa sababu kanuni zinavunjwa na watendaji wenyewe mambo haya
yanakuwa yakiumiza uoande mmoja, mtendwa huumia, na hujipanga kutumia mbinu
bora zaidi kulipiza kisasi wakati ujao.
Yanga waliwachapa bao Simba wakati walipomsainisha
Mrisho Ngassa, Simba walilalamikia lakini wakaishia kulipwa fidia, huku
mchezaji huyo akifungiwa michezo sita tu. Yalikuwa makosa, lakini si wakati wa
kuendelea kufanya mambo kwa kutumia ‘ historia mbaya ya matukio yaliyopita’.
Ngassa alitakiwa kufungiwa mwaka mmoja kama inavyotakiwa kuwa kwa kina Banda,
Okwi, na Shaffih hivi sasa lakini kama maamuzi ya busara yataendelea kutumiwa
na kanuni kuwekwa kando, mwakani viongozi wa timu nyingine watafanya hivyo kwa
sababu tayari wengine wanaruhusiwa.
0714 08 43 08
0 comments:
Post a Comment