
Na Baraka Mpenja
Imechapishwa Agosti 2, 2014, saa 9:04 alasiri
TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kesho
inashuka dimbani kucheza mechi ya marudiano dhidi ya wenyeji Msumbiji katika
uwanja wa Taifa wa Zimpeto, nje kidogo ya jiji la Maputo, kuwania kupangwa
hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kucheza fainali ya mataifa ya Afrika
mwakaini nchini Morocco.
Taifa Stars itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu
ya kutoka sare ya mabao 2-2 uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam wiki mbili
zilizopita.
Katika mchezo wa kesho, Stars inahitaji ushindi wa
aina yoyote ile au sare ya kuanzia mabao 3-3 ili kusonga mbele hatua ya
makundi.
Kocha mkuu wa Stars, Mholanzi, Mart Nooij alisema
vijana wake wapo fiti kwa ajili ya mechi ya kesho na wanaweza kuiondoa timu yake
ya zamani ya Msumbiji.
Kabla ya kutua Maputo jana, Taifa stars ilipitia
Johannesburg nchini Afrika kusini ilipoweka kambi ya siku mbili. Kambi hiyo
imeelezwa kuwa ya mafanikio kwani imewajengea imani kubwa wachezaji wa Stars.
Wakati huo huo washambuliaji wawili wa kimataifa
walioshindwa kujiunga na timu nchini Afrika kusini, wanaokipiga Tp Mazembe ya
DR Congo, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wamewasilia asubuhi ya leo mjini
Maputo tayari kwa mechi ya kesho.

Mbwana Samatta (anayemiliki mpira kushoto) amejiunga na Taifa Stars mjini Maputo asubuhi ya leo
Wanandinga hao walilakiwa na mwenyekiti wa kamati
ya ufundi ya shirikisho la soka Tanzania, TFF, Wilfred Kidau.
Samatta na Ulimwengu walionekana kuwa na furaha ya
kujiunga na Taifa Stars wakitokea mjini Lubumbashi ambapo timu yao inajiandaa
na mechi ya ligi ya mabingwa barani Afrika.
Katika
mchezo wa kwanza jijini Dar es salaam, Stars ilicheza vizuri lakini kulikuwa na
makosa kadhaa idara zote.
Safu ya ushambuliaji iliyojumuisha washambuliaji
wanne, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, John Bocco na Mrisho Ngassa alishindwa
kufunga mpaka alipoingia Khamis Mcha `Vialli` kipindi cha pili na kufunga mabao
mawili.
Bocco, Ulimwengu na Samatta kwa nyakati tofauti
walipoteza nafasi muhimu za kufunga kwenye mechi hiyo. Bila shaka mwalimu
aliliona hilo na atawatumia vizuri washambuliaji wake.
Makosa binafsi ya Kevin Yondan na Nadir Haroub `Cannavaro`
yalisababisha Stars kufungwa mabao mawili, ingawa pia lawama zinaweza
kuwaangukia Erasto Nyoni na Mwinyi Kazimoto waliojisahau kutekeleza majukumu
yao ya kuimarisha ulinzi kuanza safu ya kiungo.
Benchi la ufundi litakuwa limefanyia kazi makosa
yote na kesho litaingia na mipango ya kushinda ili kusonga mbele.

Thomas Ulimwengu (kulia) amewasili leo asubuhi mjini Maputo
Wachezaji wa Stars watakiwa kupigana kwasababu
mazingira si rafiki kwao. Wapo ugenini, watakabiliana na Msumbiji iliyopo
uwanja wake, mashabiki wake, hivyo itakuwa na nguvu zaidi ya Dar es salaam.
Lakini kama vijana watakuwa makini, wanaweza
kufanya kazi nzuri na kuibuka na ushindi au kutoa sare na hatimaye kusonga
mbele.
Mabeki watatakiwa kumlinda kiungo mshambuliaji wa
Msumbiji, Elias Gasper Pelembe. Huyu ni mchezaji hatari sana na Msumbiji
imejijenga mabegani mwake.
Ni mjanja sana, anaweza kupiga chenga na anatumia
vizuri nafasi za kufunga. An uzoefu wa 10 kuichezea Msumbiji, hivyo walinzi wa Stars
watatakiwa kumkaba vizuri kwasababu anaweza kuamua matokeo peke yake.
Kila la kheri Taifa stars. Mungu Ibariki Tanzania,
Mungu ibariki Taifa stars.
0 comments:
Post a Comment