
Kocha mkuu wa Simba sc, Mcroatia, Zdravko Logarusic hana mzaha kwenye suala la nidhamu
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
Imechapishwa Agosti 2, 2014, saa 8:24 mchana
MCHANA wa leo katika harakati zangu za kutaka
kujua nini kimetokea ulimwengu wa soka barani ulaya, nimekutana na habari ya
kocha wa FC Barcelona, Luis Enrique.
Kocha huyu alirithi mikoba ya kocha Tata Martino aliyeacha
kazi baada ya kumaliza msimu uliopita bila kikombe.
Enrique amepewa jukumu la kurudisha ufalme wa
Barcelona katika michuano ya La Liga, UEFA na ligi ya mabingwa wa dunia ya FIFA
uliopotea baada ya kuondoka kwa Pep Guardiola na kufariki kwa Tito Vilanova.
Kocha huyu amenivutia jinsi alivyokuja na mipango
mipya ya kuirudisha Barca katika hadhi yake. Moja ya maeneo aliyoyaangalia
zaidi ni nidhamu ya mpira na mazoezi kwa wachezaji.
Moja ya tatizo lililomtafuna Tata wakati anaifundisha
Barcelona ni kuwapatia uhuru mkubwa wachezaji tofauti na kipindi cha Guardiola.
Guardiola alikuwa na sheria zake binafsi na wachezaji
walipigwa faini pale walipozivunja. Lakini alipoondoka zilikufa na Tata
akazichinjilia mbali kabisa.
Enrique amefufua tena mfumo wa sheria kwa
wachezaji na kurudisha ladha ya Guardiola Barcelona.
Miongoni mwa sheria za Enrique ni kwamba mchezaji
anatakiwa kufika mazoezini saa moja kabla ya programu kuanza.
Pia wachezaji hawatakiwa kuchelewa wakati wa
chakula cha klabu. Zaidi ni marufuku kunywa pombe wakati wa Chakula kambini.
Enrique pia amewabana wazee wa bata ambapo amesema
kwamba siku mbili kabla ya mechi, wachezaji wote wanatakiwa kuwa nyumbani kabla
ya saa sita usiku. Mambo ya kukesha kwenye kumbi za starehe ni marufuku.
Hata mitandao ya kijamii kama vile Twita, facebook
na Instagram, Enrique amesema lazima wachezaji waitumie kwa njia chanya.
Enrique anasema kama mchezaji atavunja sheria hizi
atatozwa faini kuanzia Euro 1,000 na 6,000. Na akifanya makosa makubwa zaidi
anaweza kufukuzwa klabuni.
Kwa haraka haraka unagundua kuwa kwenye kundi la
wachezaji wengi wa kimataifa kuna tabia tofauti tofauti. Wapo wanaojielewa kwa
asilimia 100 na hawahitaji kusimamiwa.

Enrique (kulia) amekuja na sheria zake Barcelona
Watukutu wapo kama kawaida. Kocha hawezi kusema
lazima wachezaji wafike saa moja kabla ya mazoezi kama hawakuwepo wachezaji
wanaochelewa.
Wapo wazee wa kuzima moto. Kuchelewa ni sehemu yao
na ndio maana kocha anakuja na sheria hii.
Hata wachezaji wa kimataifa wana matatizo yao
inapofika wakati wa nidhamu. Wengine kwa jeuri kubwa ya pesa wanakesha kwenye
kumbi za starehe, na ndio maana kocha ameweka sheria ya kuwazuia kufanya hivyo
wakati wa mechi muhimu.
Mpira una miiko yake. Nidhamu ya mazoezi ni muhimu
kwa mchezaji. Kwa kocha Enrique, pengine sheria hizi zinaweza kumsaidia.
Kuna vitu vingi vya kuangaliwa ili kuibadili
Barca. Suala la mfumo wao wa `Tiki-Taka’ kuboreshwa halikwepeki. Dunia
imegundua namna ya kucheza na Barca, hivyo Enrique anatakiwa kuja na mipango
mipya ndani ya mfumo wao huo.
Sio rahisi kuua ‘Tiki-taka’ kwa Barcelona, lakini
maboresho ya mfumo huu yanahitaji ili kurudi katika kilele chao cha mafanikio.
Wakati nasoma sheria za Enrique, ikanikumbusha
wakati ule kocha wa Simba sc, Mcroatia, Dzravko Logarusic alipotua msimbazi.
Loga ni miongoni mwa makocha wa aina ya Enrique.
Anafahamu wazi umuhimu wa nidhamu ya mazoezi kwa wachezaji na nidhamu ya mpira
uwanjani.
Nakumbuka alileta sheria Msimbazi na wachezaji
wakaona kama anawazingua vile. Alisema wachezaji lazima wafike nusu saa kabla
ya mazoezi kuanza na wakifika lazima wawe wanachezea mpira na sio kukaa kupiga
domo.
Pia alisema wachezaji watakaoshuka kiwango watakwa
mshahara na wale watakaoonesha utovu wa nidhamu kwenye mazoezi watakatwa
mshahara. Wachezaji wa kibongo waliona ni utaratibu mgumu na wengine kuanza
kumuundia zengwe.
Lakini makocha aina ya Loga wanahitajika sana ili kuweka sawa nidhamu. Lazima ufuate
miiko ya soka. Umeona hata Enrique kaja na sheria zake licha ya kufundisha
klabu kubwa yenye wachezaji wakubwa.
Pia Maximo ni kocha mzuri inapofika suala la
nidhamu. Ni kocha mwenye msimamo. Kwa aina ya wachezaji wa Tanzania wasiokuwa
waumini wazuri wa nidhamu, wanaopenda kujirusha, anasa, ni muhimu kuwa na
makocha wenye mitazamio kama ya Enrique.
Makocha wa ligi kuu kujifunza sio dhambi, kama
kuna uwezekano wa kuwabana wachezaji kama anavyofanya kocha wa Barcelona kwa
sasa, inaweza kuwajenga wachezaji katika misingi ya nidhamu nzuri.
0 comments:
Post a Comment