![]() |
| Ibrahim Mwaipopo |
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
NDANDA FC ya mkoani Mtwara imegoma kujiamini
kufanya maajabu katika michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara msimu ujao mithiri
ya Mbeya City fc, lakini itajitahidi kadiri iwezavyo kuleta ushindani.
Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Ngawina Ngawina
amesema kuwa kwasasa wanaendelea na mazoezi ambapo wachezaji wanaonekana
kuimarika siku hadi siku, ingawa ni mapema kutabiri kuwa watafanya makubwa
katika msimu wao wa kwanza wa ligi kuu kwasababu mpira ni mchezo unaohitaji
maandalizi zaidi.
Ngawina alisema mpira wa miguu ni mchezo wa
hadharani na timu yenye maandalizi mazuri na mipango thabiti inapata matokeo
mazuri, hivyo kwa kutambua hilo wanaendelea kwa umakini na programu ya mazoezi,
wakianzia mazoezi magumu na sasa wanaendelea na mambo ya kimbinu na kiufundi.
Ndanda fc inayoungwa na mashabiki wengi wa mkoani
Mtwara imesajili wachezaji wapya na Ngawina amethibitisha kuwanasa wanandinga wawili
wenye uzoefu.
“Mambo yanakwenda vizuri. Tumekamilisha usajili na
tumeongeza wachezaji wawili wenye uzoefu, Thomas Morris na Ibrahim Mwaipopo”.
Alisema Ngawina.


“Tumekamilisha hatua ya kwanza ya usajili na kama
tutaona kuna mapungufu tutaongeza wachezaji wengine wakati wa dirisha dogo”
“Mwaipopo ni mchezaji ambaye hakutumika sana na klabu
ya Azam fc msimu uliopita kutokana na mipango ya mwalimu, lakini bado ni
mchezaji mzuri anayeweza kuisaidia timu yetu.”
‘Morris tumekuwa naye katika mazoezi, msimu
uliopita alicheza Kenya na sasa amerudi nyumbani, uzoefu wake utatusaidia sana.”
“Ndanda fc tunasema tutajitahidi kwa kadiri
tuwezavyo kuhakikisha tunafanya vizuri ligi kuu. Jumatano tutacheza mechi ya
kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar katika uwanja wa Bandari, hivyo itakuwa nafasi
nzuri ya kukipima kikosi chetu.’
Ndanda fc ni miongoni mwa timu tatu zilizopamba
ligi kuu msimu ujao, nyingine ni Polisi Morogoro na Stand United ya Shinyanga.
Timu zilizoshuka daraja msimu uliopita ni Rhino
Rangers ya Tabora, JKT Oljoro ya Arusha na Ashanti United ya Ilala, jijini Dar
es salaam.


0 comments:
Post a Comment