
SIKU chache baada ya timu yake kuanza ziara katika
mikoa jirani na Mbeya, Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi ametamba timu yake
itafanya maajabu ambayo yatashangaza wadau wengi wa soka nchini tofauti na
msimu uliopita.
Mwambusi alisema ana mbinu mpya kabisa
atakazozitumia kwa vijana wake huku akiwataka wapenzi na mashabiki wa timu hiyo
kutegemea mambo makubwa msimu ujao.
Kocha huyo alitoa kauli hiyo juzi Jumamosi mjini
Sumbawanga alipokuwa akizungumzia malengo na mikakati yake ya msimu ujao wa
Ligi Kuu ya Bara wakati timu hiyo ikifanya ziara ya kuwatembelea mashabiki na
wapenzi wake mikoa ya Rukwa na Katavi ikiwa ni maandalizi ya kuingia rasmi
kambini.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwambusi alisema:
“Mipango yangu ni kuiona Mbeya City inatwaa ubingwa, msimu uliopita tulikuwa na
hofu ya ugeni kwenye ligi hiyo lakini tulifanya vizuri. Msimu huu Mbeya City
inakuja kivingine kabisa wapenzi na mashabiki wetu wategemee mambo makubwa
msimu ujao.
“Baada ya kupata mialiko kutoka kwa mashabiki wetu
walioko Rukwa na Katavi ya kuwatembelea nimeona ni fursa nzuri ya kucheza mechi
za kirafiki na wenyeji ili kuweza kuangalia kasoro zilizopo kwa wachezaji wangu
kwani wametoka mapumzikoni.”
Katika msimu uliopita Mbeya City iliyoshiriki ligi
kuu kwa mara ya kwanza, ilimaliza katika nafasi ya tatu huku ikitoa changamoto
kubwa kwa timu zilizoshiriki ligi hiyo.
Chanzo:Mwanaspoti

0 comments:
Post a Comment