Na Baraka Mpenja
YANGA SC imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya
Chipukizi FC ya Zanzibar katika mchezo wa kwanza wa kirafiki uliopigwa uwanja
wa Gombani kisiwani Pemba.
Bao pekee katika mchezo huo limefungwa na Mbrazil,
Geilson Santos Santana ‘Jaja’ katika dakika ya 6 ya mchezo.
Hii ilikuwa mechi ya kwanza kwa kocha wa Yanga, Mbrazil, Marcio Maximo kuwaona wachezaji wake
wakicheza mechi ya kirafiki.
Ili kuhakikisha anawaona wachezaji wote, Maximo
alitumia vikosi viwili tofauti kwa kila kipindi.
Kipindi cha kwanza, aliwaanzisha Deogratius Munish
‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani,
Mbuyu Twite, Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Geilson Santos ‘Jaja’, Mrisho
Ngasa na Andrey Coutinho.
Kipindi cha pili Maximo aliingiza kikosi kipya
ambacho kilikuwa Juma Kaseja, Salum Telela, Edward Charles, Rajab Zahir, Said
Juma ‘Makapu’, Omega Seme, Saimon Msuva, Nizar Khalfan, Hamis Kiiza, Jeryson
Tegete na Said Bahanuzi.
Hata hivyo mabadiliko hayo hayakuweza kubadili
matokeo katika mchezo huo.
Yanga ipo kisiwani Pemba ambapo imepiga kambi
kujiwinda na msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara unaotarajia kuanza
septemba 20 mwaka huu.
Nao mahasimu wao, Wekundu wa Msimbazi Simba wapo
kisiwani Unguja kujiwinda na ligi kuu.
Msimu ujao wa ligi kuu (septemba 20), Yanga
wataanza ugenini dhidi Mtibwa Sugar katika dimba la Jamhuri mjini Morogoro,
wakati Simba wataanza na Coastal Unioni Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
0 comments:
Post a Comment