
Afisa habari na Mawasiliano wa Shirikisho la soka Tanzania, Boniface Wambura Mgoyo
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Agosti 16, 2014, saa 1:00 mchana
KLABU za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zimeendelea
kukumbushwa kuwasilisha orodha ya watendaji wa mabenchi yao ya ufundi
yakiongozwa na Kocha Mkuu katika Ofisi za Shirikisho la soka Tanzania, TFF.
Afisa
habari na mawasiliano wa TFF, Boniface Wambura Mgoyo alisema ni wajibu wa klabu
kuhakikisha zinatekeleza maagizo hayo kwani ni matakwa ya Kanuni za VPL na zile
za FDL.
“CV ni sehemu ya kanuni za ligi. Kabla ya ligi kuanza
tunahitaji kuona vyeti vya makocha wataoongoza timu za ligi kuu na daraja la
kwanza.” Alisema Wambura.
“Timu kama haina kocha anayekidhi kanuni, itakaa
bila kocha kwenye benchi lake la ufundi kwa mechi nne.”
Hata hivyo, Wambura alikiri kuwa zoezi hilo
halijakamilika kutokana na kubadilisha mfumo wa uwasilishaji ambapo sasa klabu
zinatuma orodha ya watendaji wake wa benchi la kwa njia ya kompyuta.
“Tumebadili mfumo wa uwasilishaji ambapo sasa
wanatumia kompyuta zao. Kwasasa hatuwezi kujua ni kwa kiasi gani kumekuwa na
mwitikio, lakini wameendelea kututumia na kama kuna matatizo tunawasiliana nao”.
Wambura alitoa wito kwa klabu za ligi kuu na ligi
daraja la kwanza kuendelea kutekeleza agizo hilo la kikanuni kabla ya kuanza
kwa msimu mpya wa ligi.

0 comments:
Post a Comment