
Katibu mkuu wa Shirikisho la soka Tanzania, Selestine Mwesigwa
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Agosti 16, 2014, saa 6:56 mchana
ZIARA ya Magwiji wa Real Madrid nchini Tanzania inayotarajia
kuanza Agosti 22 mwaka huu imezidi kuvuta hisia za mashabiki wa kabumbu ndani
na nje ya nchi.
Magwiji hao watakaoongozwa na wanasoka waliowahi
kutamba katika ulimwengu wa soka kwenye michuano ya La Liga, UEFA na kombe la
dunia wakiwa na Real Madrid pamoja na kombe la dunia wakiwa na nchi zao watacheza
mechi ya kirafiki Agosti 23 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam dhidi
ya kikosi maalumu cha ‘Tanzania All Stars’.
Miongoni mwa wachezaji wanaotarajiwa kuwepo ni
mwanasoka bora wa dunia wa zamani, Mfaransa Zinedine Zidane, Fabio Cannavaro,
Luis Madeila Figo na Ronaldo De Lima.

Kuelekea katika ziara hiyo ya kihistoria,
Shirikisho la soka Tanzania, TFF, limefurahishwa kuingia katika historia ya
klabu kubwa duniani ya Real Madrid ambao kwasasa ndio mabingwa wa ligi ya
mabingwa barani Ulaya.
Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa alisema hii
ni nafasi muhimu katika maendeleo ya soka la Tanzania na kama fursa hii
itatumika vizuri basi italeta matunda mazuri.
“TFF tunaingia katika historia ya Real Madrid.
Nafasi hii ni muhimu katika kuwahamasisha vijana wetu kuwa kumbe mpira unaweza
kuendelea hata baada ya kustaafu”. Alisema Mwesigwa.
“Kuna masuala tutajifunza hususani kwa wachezaji
wetu wanaostaafu mpira. Kustaafu soka si sababu ya kuacha moja kwa moja kujihusisha
na maendeleo ya michezo na kujihusisha na shughuli nyingine za kijamii.”
“Utalii na uchumi wa nchi hii pia utakuwa na kitu
cha kufaidika katika ziara hii’.
“Wito wangu kwa klabu kongwe za Simba na Yanga ni
kutumia nafasi hii kama chachu ya kuwakumbuka wachezaji wao wa zamani."

0 comments:
Post a Comment