
Na Baraka Mpenja
HATUA ya Robo fainali ya michuano ya klabu bingwa
Afrika Mashariki na kati, Kombe la Kagame, imeanza kutimua vumbi alasiri ya leo
na jioni mjini Kigali, Rwanda ambapo timu ya Polisi na APR (zote za Rwanda)
zimetinga nusu fainali.
Robo fainali ya kwanza ilianza majira ya 9:00
alasiri kwa kuwakutanisha Wanyarwanda Polisi na dhidi ya Warundi, Atletico na kushuhudia
dakika 90 zikimalizika kwa suluhu ya bila kufungana.
Sheria ya mikwaju ya penalti ikabidi itumike
kuamua mshindi ambapo Polisi waliibuka na ushindi wa penalti 9 kwa 8.
Katika mchezo huo wachezaji wote 22 walipiga penalti,
lakini Polisi ndio walikuwa na bahati zaidi.
Robo fainali ya pili ilipigwa jioni kwa
kuzikutanisha timu mbili pinzani nchini Rwanda baina ya Rayon Sport na APR.
Dakika 90 za mechi hiyo zilimalizika kwa sare ya
mabao 2-2 na APR wakashinda kwa penalti 4 kwa 3.
Katika mchezo huo zilipigwa penati 5 kwa kila timu
tofauti na mechi ya mapema.
Kwa matokeo ya mechi za leo, nusu fainali ya
kwanza itakuwa baina ya Polisi na APR.
Robo fainali nyingine zitapigwa kesho ambapo mabingwa
wa Tanzania Bara, Azam fc maarufu kama Wana Lambalamba watashuka dimbani
kukabiliana na El Merreikh ya Sudan.
Kutokana na historia nzuri ya El Merreikh katika
soka la Afrika mashariki na kati, hakika Azam wamekwaa kisiki ambacho
wanahitaji maarifa makubwa kukivuka.
Mechi nyingine ya kesho jumatano itawakutanisha
KCC ya Uganda dhidi ya Altabara ya Sudan Kusini.
0 comments:
Post a Comment