Na Baraka Mpenja,
Dar es salaam
Imechapishwa Julai 5, 2014, saa 4:54 asubuhi
TIMU ya Taifa
ya Tanzania, Taifa stars inatarajia
kutua nchini kesho (julai 6) mwaka huu ikitokea nchini Botswana ili kuendelea
na programu nyingine ya mazoezi.
Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iliweka kambi ya wiki mbili, mjini
Gaborone kwa ajili ya kujiwinda na mechi dhidi ya Msumbaji kuwania kupangwa hatua ya makundi ya kusaka
tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika, AFCON mwakani nchini Morocco.
Mechi hiyo
muhimu kwa kocha wa Stars, Mholanzi, Mart Nooij itapigwa katika dimba la Taifa,
julai 20 mwaka huu na wiki mbili baadaye mchezo wa marudiano utapigwa mjini
Maputo nchini Msumbiji.
Ikiwa ni sehemu
ya kujipima ubavu, Stars ilicheza mechi ya kirafiki siku za karibuni na wenyeji
wao Botswana na kuchapwa mabao 4-2.
Mabao ya Taifa
stars yalifungwa na Khamis Mcha `Vialli` na John Raphael Bocco `Adebayor`.
Hata hivyo,
matokeo hayo yalimfanya kocha Nooij ajue makosa ya kikosi chake na kuyafanyia
kazi kabla ya kukabiliana na Black Mambas.
Katika kambi ya
Gaborone, Taifa stars ilimkosa winga wake machachari, Mrisho Khalfan Ngassa `Anko`
aliyesafiri kwenda kufanya majaribio katika klabu ya Free State Stars
inayoyoshiriki ligi ya Afrika kusini.
Kocha Nooij
alimuita Ngassa ili acheze mechi ya kirafiki na Botswana, lakini ilielezwa kuwa
nyota huyo alikaidi na kwenda kufanya majaribio katika klabu hiyo inayonolewa
na Mbelgiji Tom Saintfiet.
Taarifa za
uhakika zinasema kuwa Nooij amemuengua Ngassa kuelekea mchezo dhidi ya Msumbiji
na tayari nyota huyo yupo nchini baada ya kumaliza majaribio yake Afrika kusini
ambapo alifuzu, lakini uhamisho wake bado ni tatizo.
Msumbiji wana
historia ya kuiharibia Taifa stars katika mechi muhimu, hivyo ni muhimu kwa
kocha kukisuka kikosi chake pamoja na watanzania kuisapoti timu yao.
Stars
ilifanikiwa kufuzu raundi ya pili ya hatua ya awali baada ya kuifunga Zimbabwe
bao 1-0 katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam na kulazimisha sare ya 2-2
mjini Harare nchini Msumbuji.
Msumbuji wao
walishinda mabao 5-0 mjini Maputo na kutoka suluhu pacha ya bila kufungana
dhidi ya Sudani Kusini ugenini.
Mshindi wa
jumla katika mechi hiyo atafuzu hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kucheza AFCON mwakani
nchini Morocco.


0 comments:
Post a Comment