
Alfredo Di Stefano hakuwahi kucheza fainali za dunia katika maisha yake ya ajabu ya soka
Na Baraka Mpenja kwa msaada wa Mtandao
GWIJI wa Real Madrid, Afredo Di Stefano ni ngumu
kumzungumzia mafanikio yake. Ni mtu aliyekuwa na kipaji kikubwa zaidi. Nyota wa
Brazil, Didi aliwahi kuulizwa swali la kuwafananisha Di Stefano na Pele ambao
wote aliwahi kucheza nao. Hapo ndipo unaweza kuanza kumzungumzia Di Stefano.
Wakati Afredo Di Stefano anawasili Madrid mwaka
1953, tayari alikuwa amejiimarisha kuwa mchezaji mzuri. Akiwa na miaka 28,
alicheza kwa kiwango cha juu akiwa nchini kwake Argentina na alishinda makombe
ya ligi akiwa na River Plate na The Copa America akiwa na timu ya Taifa.
Lakini mwaka 1949 mgomo wa wachezaji ulisimamisha
ligi ya championship ya Argentina na wachezaji wengi walienda Colombia, akiwemo
Di Stefano ambaye alitolewa kwa mkopo na klabu yake ya River Plate kwenda klabu
ya Millonarios de Bogota.
Akiwa klabu yake hiyo mpya, Di Stefano alishinda
makombe manne katika miaka minne iliyoichezea. Kiukweli, yeye na wachezaji
wenzake wakawa maarufu duniani na haikuwa rahisi kurudi kwao tena. Di Stefano, Nestor
Rossi, Julio Cozzi na Adolfo Pedernera walipokea ofa kibao kutoka nje.
Mwaka 1952 klabu yao ilialikwa kwenda Bernabeu kucheza
mechi ya kusherekea miaka 50 ya mashindano ya Real Madrid.
Wenyeji walifungwa mabao 4-2 na Millonarios na
hapo ndipo Rais wa Santiago Bernabeu alipompenda Di Stefano kwa mara ya kwanza.
Hakuwa peke yake, hata Barcelona pia walimhitaji
Muargentina huyo na wakati Real Madrid wakizungumza na Millonarios, Wakatalunya
walifanya makubaliano na wenye haki ya kummiliki kihalali Di Stefano: klabu ya River Plate.
Na hapo ndipo utata katika uhamisho ndani ya historia
ya soka la Hispania ulipoanzia na ukazaliwa upinzani mkubwa wa soka la
Hispania.
Mjadala unaendelea mpaka leo: Klabu zote zinadai
zilikuwa sahihi katika usajili huo. Real Madrid walisainiana na Millonarios,
huku Barcelona wao wakisainiana na River Plate. Baada ya miezi kadhaa ya
mabishano, mchezaji huyo alibakia jijini Barcelona akiwa hana la kufanya na
anasubiri hatima yake. Mwezi Septemba mwaka 1953, chama cha soka cha Hispania
kilifanya maamuzi na kumruhusu Di Stefano kuzichezea timu zote mbili kwa msimu
mmoja mmoja ndani ya misimu minne akianzia Barcelona, Camp Nou.
Muda mfupi baadaye, Barcelona waliwauzia haki zote
za mchezaji huyo Real Madrid. Di Stefano alisema mara nyingi kuwa Barcelona
walipoteza nia kwake baada ya kucheza mechi mbili tu na kushindwa kuonesha
kiwango kilichotarajiawa, hata katika miezi sita aliyocheza, hakucheza soka
halisia. Lakini sababu za kujiunga na Madrid hazijawahi kuzungumzwa.
Baada ya nafasi ya kujenga ushirikiano wa uchezaji
na Ladislao Kubala katika klabu ya Barcelona kuyeyuka, Di Stefano alienda Real
Madrid na alikaa kwa muda mrefu bila kutwaa kombe lolote nchini Hispania akiwa
na timu bora zaidi duniani. Lakini ghafla aliisaidia klabu kushinda makombe na
kuibadili katika soka la Hispania na Ulaya.
Katika msimu wake wa 11, Di Stefano na Merengues
walishinda makombe nane ya La Liga, moja la Copa del Rey na makombe matano
mfululizo ya Ulaya. Alifunga mabao katika makombe matano, alifikisha mabao 307
katika mechi 403 alizocheza na alionesha soka kubwa na lisilotabirika.
Juu ya hayo yote, Di Stefano kamwe hakuharibu kazi
yake uwanjani na alisaidia kuchagua wachezaji wa kuwasajili kama vile Jose
Emilio Santamaria au Hector Rial, ambao walikuwa muhimu mno kwa Real Madrid
katika utawala wake wa muongo mmoja.
Aliendelea kupata mafanikio katika mkataba wake na
Real Madrid, huku akiwa na rekodi mbaya
katika timu yake ya Taifa. Argentina hawakucheza kombe la dunia la 1950 na 1954
na alipoamua kuchukua Uraia wa Hispania mwaka 1956-nchi hiyo alishindwa kufuzu
katika fainali za mwaka 1958 na Di Stefano alipata majeruhi kabla ya fainali za
1962 (alienda Chile, lakini hakucheza). Aliishia kufunga mabao 23 katika mechi
31 alizoichezea Hispania, lakini hakuweza kutisha kama alivyofanya katika
michuano ya ligi ya nyumbani ya La Liga.
Hakika, magoli aliyofunga na makombe aliyotwaa
akiwa na Real Madrid yalimfanya awe maarufu wa kitaifa nchini Hispania.
Alipanua zaidi shughuli zake. Di Stefano
alikuwa mchezaji wa kwanza kuingia katika matangazo ya kibiashara, alitumiwa
katika nembo nyingi na alinufaika sana katika biashara hiyo. Pia alitumika
katika filamu tatu za Con los mismos
colores (1949), Once pares de botas (1954), La batalla del domingo (1963) .
Kuna mambo mengi ya kumkumbuka katika maisha yake
ya soka, lakini lingine kubwa ni lile la Hampden Park, ambapo alifunga mabao matatu
`hat-trick` kwenye mechi ambayo inasemekana kuwa bora zaidi kati ya Real Madrid
dhidi ya Eintracht Frankfurt mwaka 1960 kwenye fainali ya kombe la Ulaya. Madrid
ilishinda mabao 7-3.
Umri ukaanza kumtupa , rais wa Santiago Bernabe
ambaye hakuwa na huruma wakati anaijenga Real Madrid, alimlazimisha kumaliza
maisha yake ya soka, lakini aliondoka klabuni kwa hasira baada ya kushindwa
kuheshimiwa. Di Stefano alimalizia kucheza misimu miwili katika klabu ya
Barcelona, lakini pia akacheza Espanyol. Alistaafu akiwa na miaka 40 na kwa
haraka akaanza kazi ya ukocha, hakusomea kazi hiyo, lakini uzoefu wake
ulimsaidia.
Alizifundisha timu 9 ikiwemo Real Madrid, (mara
mbili); Valencia, (mara tatu); na cha kustaajabisha, alizifundisha klabu mbili pinzani za Argentina,
Boca Juniors na River Plate ambapo
alishinda makombe ya kitaifa.
Mwaka 2000, Rais wa sasa wa Real Madrid, president
Florentino Perez alimpa Di Stefano Tuzo ya Heshima ya Urais. Muargentina huyo
akawa balozi wa Real Madrid, na majukumu yake ya kwanza yalikuwa kupokea tuzo
ya FIFA ya klabu bora ya karne ya 20, zawadi ambayo pengine isingetokea bila
uwepo wake Real Madrid.
Mchango wake wa uwanjani, makombe aliyoshinda,
yaliifanya Real Madrid kuwa klabu bora zaidi duniani mpaka leo hii.
Umaarufu na ukubwa wa Di Stefano hauwezi kupimwa
kwa idadi ya makombe aliyoshinda, magoli aliyofunga msimu baada ya msimu,
lakini ni ukubwa wa klabu ya sasa aliyofanikiwa kuijenga.
Anastahili kuingia katika orodha ya wachezaji
wenye heshima kubwa duniani kama vile Pele, Diego Maradona na Johan Cruyff.
Pumzika kwa amani, Gwiji Alfredo Di Stefano.
Amina.

0 comments:
Post a Comment