
Wachezaji wa Yanga sasa kuanza mazoezi chini ya Maximo
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
KOCHA mpya wa Yanga sc, Mbrazil Marcio Maximo
ameanza kazi leo kwa kufanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo .
Mkutano huo umefanyika makao makuu ya klabu ya
Yanga, makutano ya Twiga na Jangwani, Kariakoo, jijini Dar es salaam.
Maximo alipata nafasi ya kuwaeleza mipango yake ya
kazi na kuwataka wachezaji waelewe umuhimu wao katika kujenga mafanikio ya
Yanga.
Kocha huyo aliyewahi kufanya kazi nchini kwa
kuifundisha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa stars, baada ya kukutana na wachezaji leo hii, sasa
yuko tayari kuanza mazoezi ya kujiwinda na msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania
bara unaotarajia kuanza mwezi agosti mwaka huu.
Pia Yanga itashiriki michuano ya kombe la kagame
na kombe la shirikisho barani Afrika baada ya kumaliza katika nafasi ya pili
msimu uliopita.
Maximo katika programu yake atakuwa na wachezaji
ambao hawako kwenye vikosi vya timu za taifa kujiandaa na michezo ya kuwania
nafasi ya kupangwa hatua ya makundi ili kusaka tiketi ya fainali za AFCON
mwakani nchini Morocco.
Baadhi ya wachezaji wa Yanga akiwemo nahodha,
Nadir Haroub `Cannavaro`, kipa Deogratius Munish `Dida`, Kelvin Yondani, Oscar
Joshua na wengineo wapo na kikosi cha Taifa stars katika kambi ya wiki mbili
mjini Gabarone, nchini Botswana.

Wakati Yanga wakifurahia na ujio wa Maximo, kwa
upande wa Simba wamekamilisha uchaguzi wao hapo jana.
Evans Elieza Aveva alishinda kwa kishindo dhidi ya
Andrew Peter Tupa na kuwa rais wa kwanza wa Simba .
Naye Goefrey Nyange `Kaburu` aliibuka kidedea
katika kinyang`anyiro cha umakamu wa rais wa klabu hiyo.
Wajumbe walioshinda na kuingia katika kamati ya utendaji
ya Simba sc ni Idd Kajuna, Coliins Friesh, Ally Suru na Saild Tully. Kwa upande
wa mwanamke ni Jasmin.
0 comments:
Post a Comment