
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Mei 30, 2014, saa 8:31 mchana
WANACHAMA wa Simba sc kuna mambo mengi
yanayoendelea kuelekea uchaguzi mkuu wa klabu yenu utakaofanyika juni 29 mwaka
huu, hasa baada ya mgombea mmoja wa Urais, Michael Richard Wambura kuenguliwa
kutokana na sababu tofauti.
Kuenguliwa kwa Wambura na kamati ya uchaguzi wa
Simba chini ya mwenyekiti wake, mwanasheria na wakala wa wawachezaji wa FIFA, Dkt.
Damas Ndumbaro kunaonekana kuvuta hisia za wadau wengi wa soka na wanachama wa
Simba wenye mapenzi makubwa kwa mgombea huyu.
Ni dhahiri wapo wanachama wengi wenye mapenzi
makubwa kwa Wambura na piga ua galagaza wao wanajua kiongozi anayeifaa Simba
kwa sasa ni huyo.
Lakini kumbuka pia kuwa wagombea wengine, Evans
Aveva na Andrew Tupa. Wote hawa wanaungwa na watu wengi nyuma yao. Lakini
yawezekana sababu zikatofautiana.
Aveva ana wapenzi wengi wanaohitaji kumuona katika
kiti cha Urais wa Simba kuanzia juni 29 mwaka huu. Ni dhahiri kuwa Aveva ni
moja ya wagombea wenye nguvu kwenye uchaguzi huu.
Ushahidi wa mamia ya mashabiki waliomsindikiza
kuchukua fomu na kurudisha fomu unatosha kuamini kuwa Aveva anaungwa mkono na
wanachama wengi, ingawa bado si rahisi kujiridhisha kuwa wote wale ni wanachama
halali wa Simba.

Wambura naye hakubaki nyuma. Siku ya kuchukua fomu
na kurudisha fomu aliambatana na wanachama wengi wanaomkubali mtu huyu. Hata
alipoengulia na kamati ya uchaguzi mwanzoni mwa wiki hii, mamia ya wanachama
walifurika mitaa ya msimbazi katikati ya wiki na kufunga ofisi za Simba kwa
madai ya kumtaka mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage kuja kutoa ufafanuzi juu ya
uhalali wa uanachama wa Wambura.
Kusimamishwa uanachana mwaka 2010 na kuishitaki
Simba mahakamani ni mapingamizi yaliyotosha kumwengua bwana Wambura.
Lakini uhalali wa nyaraka zilizomuengua Wambura,
kwasisi tulio nje ya uwanja si rahisi kujua. Wapo baadhi ya viongozi
wanaosemekana kusaini barua za kumsimamisha Wambura, lakini wanapinga kuwa
hawakuwepo siku ya kikao na sahihi zao zipo.
Sijalenga kueleza kiundani juu ya mambo haya yenye
sinema kubwa ndani yake. Lengo ni kuwakumbusha Simba baadhi ya mambo ya msingi.
Najua kuna watu wanampenda Wambura na wengine
wanampenda Aveva na Tupa. Wote wapo sahihi kwasababu ni haki yao. Katika
masuala ya demokrasia, kila mtu ana haki ya kuchagua mtu anayemhitaji.
Wanaoona Wambura anafaa, wanajua kwanini,
wanaosema Aveva anafaa wanajua kwanini, na wanaosema Tupa anafaa wanajua
kwanini. Cha msingi ni kugonganisha hoja na sera za wagombea ili mwenye mtazamo
sahihi kwa maendeleo ya klabu apatikane.
Wanachama wa Simba, tafadhali sana!, migongano
inayoendelea kwasasa isiwe kigezo cha kusahau kutafakari mambo ya msingi kuelekea
uchaguzi wenu.
Wanachama msipumbazwe na sinema zinazoendelea,
bali geukieni upande wa pili kutafakari aina ya wagombea walioomba kuingoza
Simba ili kuwa na maamuzi ya nani anafaa. Msisubiri siku ya uchaguzi ndio mkaamue,
anzeni sasa kupima upepo wa watu walioomba nafasi mbalimbali.
Bahati nzuri wengi wao walikuwepo katika uongozi
unaomaliza muda wake na wengine waliwahi kuwa viongozi miaka ya nyuma. Unaweza
kuanza kwa kupima mafanikio yao wakati wa uongozi wao, nini waliifanyia klabu
na wanakuja na lipi jipya.
Simba ni klabu kongwe yenye rasilimali nyingi.
Kama anapatikana mtu sahihi, kuna uwezekano wa kuibadili kabisa klabu hii yenye
wapenzi kila kona ya nchi hii na nje ya nchi.
Wanasimba nawakumbusheni kuwa klabu yenu inahitaji
mtu atakayesimamia mali zenu kwa manufaa ya klabu. Mtu atakayeweza kutumia
nembo yenu kwa faida ya klabu. Mtu anayeweza kutengeneza mradi wa kuuza jezi za
klabu na kuwapatia mamilioni ya fedha.
Simba inahitaji kiongozi atakayesimamia vizuri
mapato yenu ya uwanjani na fedha za udhamini mnazopata.
![]() |
Mpiganaji: Ismail Aden Rage amemaliza mambo yake Simba sc |
Simba inahitaji mtu atakayezima mianya yote ya
wachumia matumbo na kuiweka klabu kama sehemu ya kufanyia biashara zao. Simba
inahitaji mtu mwenye uwezo wa kuifanya klabu ijitegemee kimapato na kuacha
kutegemea kundi la watu fulani, hivyo wadau wawe wana nafasi ya kuchangia kama
wapenzi wa kawaida au wanachama.
Simba kwasasa haihitaji kusajili wachezaji kwa kutegemea
fedha za mtu fulani au kutumia pesa za watu wachache wenye mambo ya nyuma ya
pazia. Ifike wakati wau hawa wakisusa, klabu iwe na uwezo wa kufanya mambo
yake.
Kwasasa Simba inahitaji kuendelea zaidi kama
ilivyo kwa klabu zingine kubwa barani Afrika. Simba inahitaji mtu atakayejenga
mahusiano mazuri kati ya viongozi, wachezaji, wanachama na benchi la ufundi.
Mtu atakayekuja na mpango mzuri wa ujenzi wa
uwanja wa kisasa. Kwa rasimali ilizonazo klabu hii, hakuna hoja ya msingi ya
kutomiliki hata uwanja wa mazoezi. Wamekosekana watu wa kuunganisha nguvu ya
pamoja ili kutimiza lengo la kujenga uwanja. Mtu akayeweza kutimiza hili, ni
`lulu` kwa Simba.
Moja kati ya sehemu ambayo Simba inajipatia fedha
ni hela za getini. Lakini ukirejea mechi za mwisho mwisho katika msimu wa
2013/2014 wa ligi kuu soka Tanzania bara, klabu haikunufaika na mapato
kwasababu mashabiki walipungua mno. Chanzo ni matokeo mabaya ya uwanjani.
Nilishawahi kusema kuwa kuna uhusiano wa karibu sana kati ya uongozi bora na
mafanikio ya klabu uwanjani.
Kama viongozi wanashindwa kutekeleza majukumu yao
vizuri kwa kuwalipa wachezaji posho na mishahara kwa wakati, basi morali
itashuka kwa wanandinga wake. Wote tunajua mazingira ya kitanzania, kama
unapata hela kidogo, basi nyuma yako kuna watu wanaokutegemea.
Sasa kama klabu inashindwa kumlipa mtu
anayemsomesha mdogo wake, unadhani atafanya kazi nzuri uwanjani?.
Umefika wakati wa kuachana na mambo ya kizembe
kiasi hiki. Anahitajika watu wenye mapenzi na klabu ya Simba na si wachumia
matumbo.
Msikubali kumchagua mtu anayetaka kuifanya Simba kama
kichaka cha kufanya mambo yake au kufanikisha maslahi binafsi.
Anahitaji mtu anayeipenda klabu kwa moyo wa dhati.
Akiamushwa usiku basi neno la kwanza asema anataka kuipatia Simba mafanikio.
Atumie muda mwingi kufikiria mambo ya kuifanya Simba kuwa bora.
Yapo mengi ya kuandika, lakini haya yanatosha kwa
leo. Ukiyaangalia mambo yote hapo juu, ni rahisi kuyasoma, lakini inapofika
kumpata mtu mwenye uwezo wa kuyafanya hayo, basi unahitaji kuwa mtulivu na
kufanya tafakuri kubwa.
Kuna haja kwa wanachama wa Simba kuepukana na
siasa nyepesi zinazoendelea kwa sasa na kusahau mambo ya msingi kwa ajili ya
klabu hiyo.
Msikubali kusikia maneno ya watu wanaosema fulani hafai
au fulani anafaa. Kama kuna mtu anakueleza kuwa labda Wambura, Aveva au Tupa
ndiye anafaa, basi muulize swali moja, kwanini?
Akikupa hoja nzuri, basi timiza wajibu wako.
Kumbukeni kuna watu wanafurahia kuona timu inaingia kwenye mgogoro ili
msiwapige bao, lakini hawa wote watabainika kama wana Simba mnaweza kuwaza kwa
kina mambo yenu.
Sio mtu anakushawishi kwa hoja dhaifu kabisa ili
umuunge mkono mgombea fulani. Swala la msingi ni wewe kuwa na maamuzi binafsi
kwa faida ya klabu.
Yatasemwa mengi, yataandikwa mengi, lakini mwisho
wa siku wanachama ndio mtachambua mchele na pumba.
Kila la heri Simba kuelekea katika uchaguzi wenu.
Amani na iwe nanyi.
0 comments:
Post a Comment