![]() |
Stand United waliovalia jezi za rangi na machungwa |
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Mei 23, 2014, saa 10: 43 jioni
KUELEKEA msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania,
timu mpya iliyopanda daraja, Stand United ya mkoani Shinyanga haitafanya
mabadiliko ya aina yoyote katika kikosi
chake.
Kocha mkuu wa klabu hiyo, Fulgency Novatus ambaye
ni muumini mkubwa wa soka la vijana ameieleza
MPENJA BLOG kuwa wachezaji aliokuwa
nao ligi daraja la kwanza wataendelea kuwepo kundini isipokuwa wale tu watakaoshushwa
kikosi cha vijana chini ya miaka 20.
“Falsafa ya vijana imesaidia sana kwasababu kijana
unaweza kumwambia kitu akaelewa haraka tofauti na mchezaji mkongwe
aliyeathirika huko alikokuwa awali”. Alisema Novatus.
“Katika usajili wangu nitazingatia vijana na nitaendelea
kushikilia mfumo huu”
“Wachezaji wazoefu nao wana nafasi zao katika timu
hizi zinazoingia kwa mara ya kwanza michuano
ya ligi kuu”.
“Lakini moja ya matatizo makubwa ya wachezaji
wazoefu ni maslahi.
“Unajua timu za chini huwa zina mapato kidogo,
inapotokea mchezaji mzoefu alipita kwenye neema ya maslahi , halafu akakumbana
na ukata, anaweza kutengeneza kitu kibaya kwa wachezaji wanaokuja”.
Novatus alisema anawahitaji wachezaji wenye uzoefu
watakaoenda sambamba na matakwa yake kwa maana ya kuitumikia timu kwa moyo wa
dhati na kuamini kuwa watapata faida zaidi klabu itakapofanikiwa.
Aidha, aliongeza kuwa katika usajili wa wachezaji
wenye uzoefu, atatumia kipimo vidogo sana ambacho ni kujiuliza kule walikotoka
kulikuwa na nini na sababu ya kuondoka ni ipi.
“Timu za Dar es salaam zinahitaji wachezaji
wazuri. Mchezaji anapokuja timu kama Stand United anafuata nini?, hakuonwa na
timu za Dar?, tutakuwa makini kuangalia walikotoka kulikuwa na nini”. Alisema
Novatus.
Kocha huyo alisema anahitaji kutengeneza timu ya
ushindani na ana matumaini ya kufanya hivyo kwasababu mashabiki wao wanawapenda
na wachezaji wake wamehiari kucheza mpira kwa kuisaidia klabu yao.
0 comments:
Post a Comment